SHIRIKA la habari la Palestina WAFA limeripoti zaidi ya watu 50 wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na Israel tangu Jumamosi Alfajiri wengi wao wanawake na watoto. Watu 27 kati ya hao wameuawa katika jiji la Gaza.
Jeshi la Israel kwa upande wake limesema linafanya operesheni dhidi ya makundi ya kigaidi kwenye eneo hilo na kuwa magaidi kadhaa wameuawa.
Maandamano kupinga mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza yafanyika Berlin
Hayo yanajiri wakati maelfu ya waandamanaji wamekusanyika leo katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin, kupinga mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Maandamano hayo yaliyotarajiwa kushirikisha zaidi ya watu 30,000 yameitishwa na mashirika yasiyopungua 50.
Waandamanaji wanaitaka Ujerumani isitishe haraka kuiuzia silaha Israel, misaada iingizwe Gaza bila vikwazo na Umoja wa Ulaya uiwekee vikwazo Israel. Polisi mjini Berlin imesema imewasambaza maafisa wake 1,800 katika maeneo yote ya mji.
