Na Mwandishi wa OMH

Serikali imetoa onyo kwa taasisi na mashirika ya umma yasiyoonesha ufanisi, ikisema yako hatarini kufutwa au kuunganishwa endapo hayatachukua hatua madhubuti za kuboresha utendaji wao.

Onyo hilo lilitolewa Ijumaa, Desemba 5, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais—Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati wa ziara yake katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya kikao cha ndani na menejimenti ya OMH ikiongozwa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, Prof. Mkumbo alisema haiingii akilini kuona baadhi ya mashirika ya umma yakishindwa kutoa gawio stahiki licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.

Alisema Serikali itatoa muda maalum kwa taasisi husika kujirekebisha kabla ya kuchukua maamuzi ya kuyaunganisha au kuyafuta pale itakapobidi.

“Ni afadhali kuwa na mashirika machache ya biashara, lakini yanayotoa gawio stahiki kwa Serikali,” alisisitiza Prof. Mkumbo, ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Dk. Pius Stephen Chaya, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Tausi Kida.

Kwa mujibu wa OMH, Serikali inamiliki hisa katika taasisi na kampuni 308, ambapo 91 pekee ndizo zinazofanya biashara na 217 hazifanyi.


Prof. Kitila alisema Serikali inataka kuona wananchi wakifaidi matunda ya uwekezaji wake wa Sh92.3 trilioni uliofanywa katika mashirika ya umma.

Katika mwaka wa fedha 2024/25, OMH ilikusanya Sh1.028 trilioni kama gawio kutoka kwa taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache — kiasi kilicho rekodi historia mpya tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo mwaka 1959.

Hata hivyo, Serikali inaamini bado kuna nafasi kubwa ya kukusanya zaidi.

Kwa muktadha huo, Serikali imeiwekea OMH lengo la kukusanya Sh1.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26, huku ofisi hiyo yenyewe ikijiwekea lengo la ndani la kukusanya hadi Sh2 trilioni kutokana na mageuzi inayoyasimamia kwenye mashirika ya umma.

Prof. Mkumbo alisema kwamba Serikali itaongeza ufanisi zaidi kwa kuhakikisha upatikanaji wa watendaji na wajumbe wa bodi za mashirika ya umma unafanyika kwa uwazi na ushindani.

“Kazi yangu ni kuhakikisha tunakuwa na Sheria bora ya Uwekezaji wa Umma itakayo chochea ufanisi wa mashirika ya umma,” alisema.

Alisema anaamini maboresho ya muswada huo yatafanyika kwa haraka na hatimaye kusomwa kwa mara ya pili bungeni katika siku za karibuni.

Aidha, alibainisha kuwa lengo la Serikali ni kubadili sura, ufanisi na utendaji wa mashirika ya umma ili yaweze kutoa huduma bora na kuchochea uwekezaji.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema OMH imejipanga kuendelea kuimarisha mashirika ya umma ili kuongeza ufanisi katika huduma na uwekezaji.

“Usimamizi bora wa utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma ni chachu ya mageuzi katika uendeshaji wa sekta hii,” alisema Bw. Mchechu.

Aliongeza kuwa uimarishaji wa usimamizi huo utaongeza uzalishaji, kuboresha uchumi na kuongeza mapato ya kodi na yasiyo ya kodi — ambayo ni muhimu katika kuwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake.