Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Zaidi ya mashirika 10,717 yasiyo ya kiserikali (NGOs) yamesajiliwa nchini hadi kufikia Aprili 2025, ikiwa ni ongezeko la mashirika 1,202 yaliyosajiliwa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025. Kati ya hayo, mashirika ya kimataifa ni 42, ya kitaifa 1,107, kimkoa 29 na kiwilaya 24.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameeleza hayo Bungeni leo Mei 27,2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2025/2026 na kueleza kuwa Mashirika haya yamekuwa mstari wa mbele katika kuchochea maendeleo katika sekta za afya, elimu, mazingira, maji, nishati, kilimo na utawala bora.

Dkt. Gwajima ameeleza katika kipindi hicho, Mashirika 507 yalifanyiwa ufuatiliaji katika mikoa 15 nchini, yakiwemo Iringa, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza, kati ya mashirika 8,052 yaliyoko katika mikoa hiyo lengo lilikuwa kufuatilia uzingatiaji wa sheria na utekelezaji wa miradi ya vipaumbele vya kisekta ikiwemo elimu ya ufundi, rasilimali maji, kilimo, na mazingira.

Amesema miradi iliyotekelezwa imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii,Miongoni mwa miradi hiyo ni nyumba 271 zilizojengwa kwa kaya masikini mkoani Iringa na Karakana 2 za ufundi stadi ikiwa ni pamoja na huduma ya maji safi kwa watu 38,798.

“Manufaa mengine ni Mikopo na uongezaji thamani kwa zaidi ya vikundi 5,000 vya wakulima, wakiwemo vijana na watu wenye ulemavu, aidha mashirika 46 kati ya yaliyofuatiliwa yanatekeleza Mpango Mkakati wa Uendelevu kwa kutumia miradi kama mashamba darasa, vituo vya mafunzo, mashine za kusaga, hosteli, ufugaji wa nyuki, na visima vya maji, ili kujitegemea kifedha, “ameeleza.

Katika upande wa fedha, Waziri huyo ameeleza kuwa kwa mwaka 2024/2025, Wizara iliridhia mikataba 478 ya ufadhili yenye thamani ya Shilingi bilioni 561.8, ukilinganisha na mikataba 192 ya bilioni 205.8 mwaka uliopita – ongezeko la zaidi ya mara mbili ambapo fedha hizo zinalenga miradi ya afya, elimu, haki za binadamu, kilimo, maji na utawala bora.

“Wizara pia imeboresha Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika ya mwaka 2020 na kuchapisha toleo jipya la mwaka 2024, linaloainisha majukumu ya Serikali Kuu na TAMISEMI, sambamba na miongozo ya mila na desturi, maadili ya Kitanzania, na ushirikiano wa maendeleo, ” Amesema.

Licha ya hayo amesena zaidi ya mashirika 117 yaliyokuwa kwenye uangalizi maalum yameondolewa baada ya kurekebisha upungufu wa uzingatiaji wa sheria, huku mashirika 94 yakiendelea kufuatiliwa. Ufuatiliaji huo umeenda sambamba na mafunzo juu ya miongozo mbalimbali ikiwemo ushiriki wa NGOs kwenye bajeti ya serikali.

“Kwa sasa, mfumo wa kidigitali wa utambuzi wa mashirika haya unapatikana kupitia Simujanja, jambo linalowawezesha wananchi kuyafuatilia kwa uwazi zaidi, ” amesema.