Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi, ameitaka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuendelea kuwekeza zaidi katika mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi popote walipo.

Bw. Maswi ametoa wito huo wakati wa hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu Barani Afrika yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma, tarehe 10 Agosti 2025.

“Licha ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika matumizi ya teknolojia , naiomba RITA kuendelea kuwekeza zaidi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zaidi kwa wananchi,” amesema Bw. Maswi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi (katikati) akimkabidhi cheti cha kuzaliwa mmoja wa wazazi (kushoto) aliyeudhuria kwenye hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na takwimu Barani Afrika yanayoadhimishwa kila mwaka Mwezi Agosti, yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nanenane Jijini Dodoma. kulia ni Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bw. Frank Kanyusi na wapili kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya RITA, Bw. Erick Kitali.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: ‘Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ni Msingi wa Miundombinu ya Kidijitali ya Umma na Mifumo ya Kidijitali ya Utambuzi wa Kisheria Barani Afrika’.

Amesema kuwa dunia ya sasa inaendeshwa na teknolojia, hivyo Tanzania haiwezi kubaki nyuma.

Amesema kuwa usajili wa RITA wa matukio muhimu kwa njia ya kidijitali huleta manufaa makubwa ikiwemo kusaidia mfumo huo kusomana na mifumo mingine ya kitaifa kama vile wa kitambulisho cha taifa (NIDA), afya na elimu.

Kwa mujibu wa Bw. Maswi, tangu kuzinduliwa kwa Mpango wa ‘Digital CRVS System’ mwaka 2022, zaidi ya kumbukumbu milioni 3 zimeingizwa katika mfumo wa kidijitali, hatua ambayo imeimarisha usalama na upatikanaji wa taarifa kwa haraka.

Mafanikio haya, amesema, yanatokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya TEHAMA, mafunzo kwa watumishi wa umma, na juhudi za uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni urithi wa kitaifa, ni alama ya heshima kwa kila raia na ni injini ya maendeleo ya Taifa,”

“Bila takwimu sahihi hatuwezi kupanga kwa ufanisi, mipango ya maendeleo, au kutathmini changamoto zinazotukabili,” amesema.

Ametoa wito kwa serikali za mitaa, sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo kuendelea kushirikiana na RITA kuhakikisha kuwa kila tukio la kuzaliwa, ndoa, talaka, kifo au uasili wa mtoto linarekodiwa kwa njia ya kisasa, salama na sahihi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya Usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na takwimu Barani Afrika yanayoadhimishwa kila mwaka Mwezi Agosti kumalizika, yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nanenane Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bw. Frank Kanyusi.

Awali, akitoa maelezo kuhusu hafla hiyo, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu ni ya nane tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018, yakiwa na lengo kuu la kuongeza uelewa na kasi ya usajili wa matukio muhimu kama kuzaliwa, ndoa, talaka, vifo na watoto wa kuasili mara yanapotokea.

“RITA kama taasisi yenye jukumu la kusimamia na kuratibu usajili wa matukio haya nchini, imeendelea kuweka mikakati na kuendesha programu mbalimbali kuhakikisha tunaongeza kasi ya usajili, huku msingi wetu mkubwa ukiwa ni matumizi ya mifumo ya kidijitali,” amesema Bw. Kanyusi.

Ameeleza kuwa kupitia mfumo wa ‘eRITA’, wananchi sasa wanaweza kutuma maombi ya huduma bila ya kufika katika ofisi za wakala, na badala yake huchagua wilaya iliyo karibu kwa ajili ya kuchukua cheti cha huduma aliyoomba kwa wakati.

Maadhimisho hayo yameendelea kusisitiza umuhimu wa TEHAMA katika kujenga mifumo thabiti ya usajili, yenye uwezo wa kutoa huduma bora, sahihi na kwa wakati kwa kila Mtanzania.