Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Katika kilele cha safari ya ndoto ya muda mrefu, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameweka historia kwa kuzindua rasmi jengo la kupumzikia ndugu wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodomamradi aliouota tangu mwaka 2010.

Uzinduzi wa jengo hilo ulifanyika Juni 25, 2025, ukihudhuriwa na wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, ambapo Mavunde ameeleza kwa hisia namna tukio la kushuhudia wananchi wakiishi nje ya geti la hospitali usiku mmoja lilivyomgusa hadi kugeuka ndoto ya maisha yake ya kisiasa.

“Nilitamani sana siku moja nipate nafasi ya kuongoza katika eneo nilikozaliwa ili niweze kuleta mabadiliko ya kweli. Nilishuhudia watu wamelala chini, wanawake, wanaume na watoto, wakichanganyika nje ya hospitali bila msaada.

Nilijiambia, ‘ikiwa nitapata nafasi, hii siwezi kuiacha hivihivi’,” amesema Mavunde kwa sauti ya faraja kwa kutimiza azimio hilo.

Jengo hilo lenye mabenchi 24, televisheni kwa ajili ya taarifa, na uzio wa kiusalama, limejengwa mahsusi kwa ajili ya kuwapunguzia machungu na changamoto ndugu wa wagonjwa wanaotoka mikoa mbalimbali kufuata matibabu Dodoma jambo ambalo Mavunde amelieleza kuwa ni wajibu wake kwa jamii.

Aidha, Mavunde ameeleza kuwa tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015, amekuwa akitekeleza falsafa ya kuwa “mtumishi wa watu” na si kiongozi wa hadhi pekee.

Ameweka kumbukumbu ya mfumo wa kidijitali aliouanzisha mwaka 2017 kuhakikisha uwajibikaji kwa watumishi wa afya kwa kufunga kamera na maikrofoni katika maeneo ya kutolea huduma.

Katika hatua nyingine, ametumia nafasi hiyo waomba viongozi wa Jiji la Dodoma kuwaangalia kwa huruma akinamama wanaofanya biashara ya chakula eneo la hospitali hiyo kwa kuwapatia maeneo rasmi na yenye kivuli ili kuboresha mazingira yao ya kazi, akiahidi kuwasaidia kwa hali na mali.

Mavunde pia ameshukuru wadau waliomsaidia kutimiza ndoto hiyo, akiwemo Mkurugenzi wa Asasi ya Salim Asasi, wachezaji wa klabu ya Yanga Stephane Aziz Ki na Djigui Diarra, pamoja na mfanyabiashara Vencampan, ambao wote kwa pamoja walichangia zaidi ya asilimia 80 ya gharama za ujenzi wa jengo hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemery Senyamule, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alieleza kuwa jengo hilo linafungua ukurasa mpya wa matumaini kwa familia nyingi, na kwamba ni mfano halisi wa siasa ya matendo inayogusa maisha ya wananchi.

“Mhe. Mavunde amefanya jambo lenye uzito mkubwa kwa jamii,hii ndiyo maana halisi ya kiongozi wa kuigwa kwa kuwapa wananchi wake ahueni katika kipindi kigumu cha kuuguza wapendwa wao,” amesema Senyamule.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ibenzi Ernest, ameeleza kuwa mchango huo umeongeza thamani kubwa kwa hospitali hiyo ambayo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa watumishi na uzio wa kuzunguka hospitali nzima.

“Tuna dira ya kutoa huduma bora kwa kila mwananchi, na jengo hili limetuongezea nguvu na matumaini. Mchango huu unaonesha kuwa viongozi wetu wana usikivu na moyo wa kushirikiana katika kuboresha huduma za afya,” ameeleza Dkt. Ernest.