Waziri Wa Madini na Mbunge wa Mtumba, Anthony Mavunde, amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya nje imesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuachiwa kwa dereva wa gari la mzigo, Juma Maganga, aliyekuwa amefungwa nchini Sudan Kusini baada ya kumgonga mwanajeshi na kupoteza maisha.

‎Mhe. Anthony Mavunde ameyasema hayo tarehe 3 Januari, 2025, Jijini Dodoma.

‎Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kumpokea Juma Maganga alipokuwa anawasili nyumbani kwake Dodoma,, Waziri wa Madini na Mbunge wa Mtumba, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje iliingilia kati kesi hiyo na kuleta uhueni kati ya Serikali ya Tanzania na Sudan Kusini.

‎Aidha amebainisha kuwa hatua hiyo ilisaidia Nchi ya Sudan Kusini kuona kuwa Serikali ya Tanzania ipo nyuma ya raia wake katika kuhakikisha haki inapatikana.

‎Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa malipo ya dola 1,500 yalifanyika katika Mahakama ya Juba, Sudan Kusini, tarehe 29.12.2025, hatua iliyofungua njia ya kuachiwa kwa Juma Maganga.

‎Aidha amebainisha kuwa tarehe 31.12.2025 Juma Maganga aliachiliwa huru na kuanza safari ya kurejea nyumbani Dodoma, Tanzania.

‎Amesema kuwa tukio hilo lilitokana na ajali iliyotokea tarehe 14.02.2025 nchini Sudan Kusini, ambapo Juma Maganga aliyekuwa dereva wa gari kubwa alimkonga mwanajeshi mmoja aliyepoteza maisha, hali iliyopelekea Juma kushikiliwa na vyombo vya sheria vya nchi hiyo.

‎Aidha amebainisha kuwa Juma alitakiwa kulipa faini ya ng’ombe 51 sawa na shilingi 36,000,000 za Kitanzania kwa mujibu wa mila na desturi za Sudan Kusini, ambapo marehemu aliacha wake watatu pamoja na wazazi wake waliotakiwa kufikiwa na mgao.

‎Kwa upande wake, Dereva Juma Maganga amesema kuwa alipitia nyakati ngumu sana alipokuwa gerezani, akieleza kuwa kila aliyekuwa anajitolea kumsaidia alitishiwa kuuawa.