Mawakala takribani 120 kutoka nchini Marekani wamefurahishwa na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania ikiwemo utajiri wa utamaduni mzuri, wanyamapori na mandhari inayovutia.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Excellent Guide Tours and Safaris, Bw. Justin Alfred usiku wa Novemba 7,2025 katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mawakala hao waliowasili nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

“Tuna furaha sote tumeweza kutalii kwa kuona wanyamapori kama tembo, twiga, simba,nyati na wengine na nipende kuiambia dunia kuwa Tanzania ni nchi salama na ina watu wakarimu hivyo wasisite kuja kuitembelea” amesema Bw. Alfred.

Amefafanua kuwa lengo la ziara hiyo ya mawakala nchini Tanzania ni kuhakikisha dunia yote inafahamu kuhusu Bara la Afrika hasa nchi ya Tanzania kutokana na utajiri wake na vivutio ilivyonavyo.

Naye, Wakala wa Utalii kutoka kampuni ya Nexion Travel ya Marekani, Patricia Walker alisema yalikuwa ni matamanio yake tangu akiwa na umri wa miaka mitano kuitembelea Tanzania hasa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo amefurahishwa na ukarimu na huduma zilizotolewa tangu awasili nchini na kwamba amepata kumbukumbu isiyosahaulika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi amewashukuru mawakala hao wa utalii kwa kuitembelea Tanzania na kuwahimiza kuwa mabalozi wazuri wa utalii wanaporudi nchini kwao.