Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamefanya mkutano kwa njia ya video na kutangaza kuiunga mkono Ukraine kabla ya mkutano kati ya rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin huko Alaska.
Kauli mbiu ya mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ilitolewa na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja huo Kaja Kallas aliyesema kuwa mshikamano wa kuisaidia Ukraine na kuzidisha shinikizo kwa Urusi vinahitajika ili kumaliza vita na kuzuia uchokozi wowote wa baadaye wa Urusi barani Ulaya.
Kallas amesema Umoja huo unaandaa kifurushi kipya na cha 19 cha vikwazo kwa Urusi, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Kallas amesisitiza kwamba kwa kuwa Urusi haikukubali mpango wa kusitisha mapigano bila masharti, hakuna makubaliano yoyote yanayopaswa kujadiliwa bila kuishirikisha Ulaya.
