MEXICO imethibitisha kuwa wanajeshi wamemuua mbabe wa ulanguzi wa dawa za kulevya ambaye alikuwa mmoja wa watu wanaosakwa sana nchini humo na Marekani. Nemesio Oseguera “El Mencho, alikuwa na umri wa miaka 59.

Jeshi limesema Nemesio Oseguera, kiongozi mwenye umri wa miaka 59 wa mtandao wa Jalisco New Generation, alijeruhiwa katika mapigano na wanajeshi katika mji wa Tapalpa na kufariki alipokuwa akisafirishwa hadi Mexico City. Mamlaka zilikuwa zimetangaza zawadi ya dola milioni 15 za Marekani kwa yeyote mwenye taarifa za aliko.

Watu wenye silaha waliokuwa wakilipiza kisasi kwa uvamizi huo walifunga zaidi ya barabara 20 katika jimbo la magharibi la Jalisco, unakopatikana mji wa Tapalpa, kwa magari na malori yaliyochomwa moto. Vurugu hizo zilienea hadi majimbo mengine pia.

Oseguera, aliyejulikana kama “El Mencho,” ni mmoja wa wababe wakubwa wa dawa za kulevya wa Mexico walioangushwa tangu kukamatwa kwa waanzilishi wa genge la Sinaloa, Joaquin ‘El Chapo’ Guzman na Ismael Zambada. Wote wawili sasa wanatumikia kifungo nchini Marekani.

Taarifa ilisema pamoja na ujasusi wa kijeshi wa Mexico, uvamizi huo ulifanywa kwa “taarifa za ziada” kutoka kwa serikali ya Marekani. Ilisema watu sita wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi hilo waliuawa na wanajeshi watatu walijeruhiwa.