Na Baltazar Mashaka, JamhuriMedia, Mwanza
WAZIRI wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza–Isaka chenye urefu wa kilomita 341, unaotarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Akizungumza katika eneo la Fella, wilayani Misungwi, leo Februari 24, 2026, baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 68 na unaendelea vizuri.
Alisema mradi huo wa kimkakati unaogharimu dola za Marekani bilioni 1.326 (takribani shilingi trilioni 3.06), ni mkubwa na kielelezo cha kujivunia, huku akimshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wake, akieleza kuwa wakati anaingia madarakani mradi ulikuwa hatua sifuri sasa umefikia hatua kubwa.
Kwa mujibu Profesa Mbarawa, jengo la stesheni kuu ya Mwanza lenye uwezo wa kuchukua abiria 900 pamoja na majengo mawili ya biashara ujenzi unaendelea vyema, miundombinu ikiwemo madaraja ikifikia takribani asilimia 90, huku ulazaji wa mataruma ukiwa asilimia 53.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa fedha ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vya kimataifa na kwa kuzingatia thamani ya fedha, una uwezo wa kuhimili changamoto mbalimbali ikiwemo matetemeko ya ardhi.
Profesa Mbarawa aliwashukuru wananchi wa Mwanza kwa shughuli za maendeleo na kuunga mkono mradi huo, akibainisha kuwa eneo lililosalia na changamoto ni Mkuyuni ambako kuna makazi yanayochelewesha ulipuaji wa miamba.
Hata hivyo, alisema kuwa, mkandarasi ameahidi kukamilisha kazi hiyo ifikapo Agosti mwaka huu na kuanza uwekaji wa njia ya reli huku akionya waliopata kazi katika mrad huo wasifanye mambo ya ovyo ikiwemo wizi wa malighafi ya saruji, nondo na vyuma, wataakuwa wanawaiba Watanzania si mkandarasi.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa mbalimbali zikiwemo ujenzi wa Bandari Kavu ya kuhifadhi mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kubadilisha vichwa vya treni na mabehewa, na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo la Misungwi, aliwataka wananchi kutunza mali za mradi na kuepuka vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi.
Mbunge wa Misungwi, Silvery Salvatory (CCM), alisema reli ya SGR itaongeza usafirishaji wa mizigo ya ndani na kutoka nchi jirani, hivyo kuchochea uchumi jumuishi kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,alitoa wito kwa wananchi kujipanga kunufaika na fursa zitakazotokana na miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi, alisema miradi ya SGR, Bandari Kavu na Daraja la JPM itaimarisha uchumi wa wilaya hiyo na kuwataka wananchi kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro na madai ya fidia baadaye.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisema kukamilika kwa reli ya SGR kutaufungua mkoa wa Mwanza kiuchumi na kuongeza fursa za uwekezaji.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Masanja, alisema eneo la Misungwi limepangwa kuwa kitovu cha shughuli za kilojistiki, na kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa za kuwekeza katika Bandari Kavu, ambayo serikali imeiachia sekta binafsi kuendesha.
Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 treni ya SGR inasafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ikiwa na mizigo na abiria, na hivyo kuimarisha uchumi wa taifa.





