Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga

Polisi mkoani Shinyanga inamshikilia Pendo Medusela (37), mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Timithoy Magesa (35), kwa kumkatakata kwa wembe sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kile kilichodaiwa ni kutokana na wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo amnalo lilitokea Agosti 23, mwaka huu, majira ya saa 3 usiku, katika nyumba ya kulala wageni ya Bwashee, iliyopo Ndala Manispaa ya Shinyanga.

Amesema kabla ya mauaji hayo, mtuhumiwa Pendo alipigiwa simu na mwanamke mwingine kwa kutumia simu ya marehemu, akimuonya aachane naye kwa madai kwamba ndiye anayempenda.

Baada ya muda marehemu alimtafuta Pendo na kumtaka wakutane katika nyumba hiyo ya wageni ili wazungumze suala hilo.

“Hata hivyo, walipokutana walianza kugombana kuhusu mwanamke aliyempigia simu, hali iliyosababisha Pendo kutumia wembe aliokuwa nao kumkatakata Timothy sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha kuvuja damu nyingi,” amesema Kamanda Magomi.

Ameongeza kuwa, marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.

Hata hivyo Kamanda Janeth ameiasa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake wafuate sheria ili kupata haki.