Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Marry Timotheo, Mkazi wa Garijembe Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya Mtoto wake aitwaye Scola Athanas Mwaba [10] aliyekuwa Mwanafunzi wa Darasa la Nne katika Shule ya Msingi Ngonde.
Tukio hilo limetokea Desemba 09, 2025 saa 6:30 mchana katika Kijiji cha Garijembe, Kata na Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya baada ya Marry Timotheo [Mama mzazi wa marehemu] kumuadhibu kwa kumpiga kwa kitu kizito kichwani kwa madai ya utukutu.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kujichukulia ni sheria mkononi kwa kumuadhibu mtoto wake kwa kumpiga hadi kufa na kisha kuutupa mwili wake shambani jirani na nyumba yake kwa kushirikiana na jirani yake aitwaye Sharifa Nzalanje, Mkazi wa Garijembe ambaye pia anashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Upelelezi unakamilishwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wazazi na walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa kutoa adhabu kali kwa watoto na badala yake watoe adhabu za kuwarekebisha na kuwafundisha mienendo na maadili mema ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata ikiwemo kupoteza maisha au kupata ulemavu.


