Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amesema kuwa changamoto kubwa inayolikumba Bara la Afrika si ukosefu wa sera nzuri bali ni uhaba wa viongozi wenye uwezo wa kuzitekeleza.
Akizungumza wakati wa Mhadhara wa Siku ya Afrika uliofanyika Dar es Salaam leo, Mbeki amesitiza kuwa bara lina maono makubwa, lakini hatua za kuyafanikisha hazipo kwa kiwango kinachohitajika.
Mbeki alieleza kuwa alipaswa kustaafu rasmi mwaka 2009, lakini kutokana na hali ya kisiasa nchini mwake, aliondoka madarakani mwaka mmoja mapema.
Hata hivyo, baadhi ya wenzake walimshauri aendelee kushughulikia masuala ya bara la Afrika baada ya kustaafu, hasa katika eneo la uongozi na utekelezaji wa sera.
Kutokana na ushauri huo, amesema alianzisha Taasisi ya Uongozi wa Afrika kupitia Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA). Taasisi hiyo inalenga kuwajengea uwezo viongozi wa Afrika ili waweze kusimamia na kutekeleza sera mbalimbali zinazolenga maendeleo ya bara. Alisema UNISA ilichaguliwa kwa sababu ni taasisi ya masafa inayofikia zaidi ya nchi 40 za Afrika.

Mbeki amesema kuwa taasisi hiyo na mihadhara ya Siku ya Afrika si ya Afrika Kusini pekee bali ni ya bara lote. Alisema ni muhimu mihadhara hiyo kuzunguka katika nchi tofauti ili kuwahusisha Waafrika wengi zaidi katika mijadala ya maendeleo ya bara lao. “Hii ni taasisi ya Kiafrika, si ya taifa moja,” alisisitiza.
Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mhadhara wa Siku ya Afrika kwa mara ya tatu, ikimkaribisha Mbeki pamoja na viongozi wengine mashuhuri waliowahi kutoa mihadhara hiyo akiwemo hayati Rais Benjamin Mkapa. Mbeki amesema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo mara tatu.
Ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa Afrika kuchukua hatua za vitendo badala ya kuishia kuwa na ndoto au maono yasiyo na utekelezaji.







