Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi kimesema kitashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu kwa mujibu wa sheria na taratibu za kidemokrasia kwani hakuna sababu ya CCM kushindwa Visiwani Zanzibar .

Katibu wa Kamati Maalum ya Nec Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ,Khamisi Mbeto Khamis, ameeleza hayo baada ya mgombea Urais wa CCM, Rais Dk Hussein Ali Mwinyi alipohutubia maelefu ya wana CCM na Wananchi.

Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni za CCM kwa Zanzibar ,zimezinduliwa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Mwenyekiti Mao Tse Tung, Kisiwani Unguja.

Mbeto alisema Ushindi wa CCM hauna kizuizi chochote baada ya serikali ya Awamu ya Nane kutimiza wajibu wa kuwatumikia wananchi chini ya serikali ya Rais Dk Mwinyi.

Alisema haiba ya Ustawi wa Maendeleo inayoonekana Unguja na Pemba ,ni tiketi itakayokipatia Ushindi wa kishindo CCM Mwaka 2025-2030.

“CCM hakina sababu ya kushindwa Uchaguzi huu . Kimetekeleza kwa vitendo Sera zake kwa ufanisi na viwango stahili ” Alisema Mbeto

Aidha, Katibu huyo Mwenezi ,aliongeza kusema kwa CCM ni fahari kuona idadi kubwa ya Wananchi, wakiendelea kukiunga mkono , kukuamini , kukipenda na kukitegemea .

“Siri ya ushindi wa chama chochote makini cha Siasa ni maandazi ya kimkakati , kioganaizesheni na kujipanga .Tumejiandaa kisawasawa ,sasa tuko tayari kwa ushindi wa kidemokrasia ” Alieleza

Katibu huyo Mwenezi akijigamba mbele ya Waandishi wa habari, amesifu kazi kubwa iliofanywa na SMZ, miaka mitano iliopita chini ya Utawala wa Dk Mwinyi.

Alisema CCM kitashinda kwa Asilimia 85 ya kura za Urais, hivyo Mgombea wake Dk Mwinyi , atarudishwa tena madarakani kwa ridhaa ya Wananchi .

“Kielelezo cha ushindi wetu ni matokeo ya kufanikisha kazi za kimaendeleo . Mafanikio yaliopatikana katika Sekta za Elimu , Miundombinu, Ustawi wa Jamii , Miradi ya Kiuchumi, Barabara za lami , Usafiri wa Anga , Biashara na Utalii kwa ccm ni funguo ya ushindi “Alisisitiza .

Mbeto alisema kimsingi Utendaji wa Serikali ya Awamu ya Nane, umezikonga nyoyo za Wananchi pia kuwavutia hata wageni wanaotembelea Visiwani humu.