Na Mwandishi Wetu , JamhuriMedia,Mbeya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya (Mbeya DC) imeibuka mshindi wa kwanza wa kikanda katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, zilizohitimishwa mkoani Mbeya, hatua iliyopongezwa na viongozi mbalimbali wa serikali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, alikabidhi zawadi hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayopitiwa na Mwenge wa Uhuru.

Zawadi hiyo ilipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Erica Yegella.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bi. Yegella amesema siri ya ushindi huo ni matokeo ya kazi ya pamoja, uzalendo na utayari wa kupokea ushauri kutoka kwa viongozi wa ngazi mbalimbali.

“Kweli namshukuru Mkuu wetu wa Mkoa, Beno Malisa, na Mkuu wa Wilaya, Solomon Itunda, ambao hawakusita kushirikiana nasi usiku na mchana katika kufanikisha shughuli za Mwenge wa Uhuru.

Amesema ni jambo la kipekee kuona viongozi wa ngazi hiyo wakikesha nasi hadi asubuhi — nyota yetu ilianza kung’aa tangu mwanzo,” Amesema Yegella.

Ameongeza kuwa ushindi huo umefungua ukurasa mpya kwa Halmashauri hiyo katika kuimarisha utendaji na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, huku akiwapongeza watumishi wote wa Halmashauri kwa bidii, mshikamano na kujituma kwao.

“Moto huu ulioanzishwa, tuendelee nao. Ushindi huu ni wetu sote,” amesisitiza Yegella.