Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Jamii imetakiwa kuongeza uelewa juu ya namna ya kutambua noti bandia na kuhakikisha zinatunzwa kwa usahihi ili kulinda thamani ya Shilingi.
Hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza gharama ambayo Serikali hutumia mara kwa mara kuchapisha noti mpya, jambo ambalo lingeepukika endapo wananchi wangezingatia matumizi sahihi na uangalifu katika mzunguko wa fedha.

Wito huo umetolewa leo November 21,2025 Jijini hapa na Afisa Mwandamizi wa Benki kuu ya Tanzania (BoT)Atufigwege Jampion Mwakabalula katika mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti ambapo ameeleza kuwa changamoto kubwa bado ipo kwenye jamii kutokana na kukosa uelewa wa alama za usalama .
Kwa mujibu wa wataalam huyo ,sehemu kubwa ya wananchi hukubali na kuzungusha fedha bandia kwa bahati mbaya, kwa kuwa hawajui namna ya kuzitambua kwa kutumia mbinu rahisi zinazopatikana kwenye kila noti halisi.
Pia amesema kuwa mzunguko wa noti bandia unaigharimu Serikali kwa kuharibu utulivu wa uchumi na kulazimisha uchapishwaji mpya wa fedha kwa gharama kubwa na kwamba fedha hizo zingeelekezwa kwenye afya, elimu au miundombinu huishia kutumika kuziba pengo linalotokana na mzunguko wa noti zisizo halali.

Kutokana na hayo amewahimiza wananchi kuzitunza noti kwa njia sahihi ili zidumu muda mrefu kwa kuepuka kuzikunja mara kwa mara, kuzihifadhi kwenye pochi au sehemu isiyobana, kuepuka kuzilowesha kwa maji au kuziweka kwenye joto kali, na kutoweka alama, kutoboa au kuchora kwenye noti.
Amefafanua kuwa uharibifu wa noti unaosababishwa na uzembe wa watumiaji ndio unaoongeza zaidi gharama kwa Serikali, kwani noti zilizoharibika hutolewa kwenye mzunguko na kuchapishwa upya.
“Kila noti ya Tanzania ina alama za kiusalama ambazo ni ngumu kuiga ambazo ni pamoja na kivuli cha picha (watermark) kinachoonesha sura ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na thamani ya noti husika,
Alama nyingine ni za vipande vipande (see-through register) zinazoonesha tarakimu kamili ya thamani ya noti inapomulikwa kwenye mwanga; na alama ya kivuli kilichofichika (latent image) ambayo huonekana kuwa angavu noti inapogeuzwa upande mbalimbali, “amesema.

Aidha, wananchi wameelekezwa kutambua pembezoni mwa noti kuna alama zinazoparuza (tactile corners) na alama maalum za kuwasaidia watu wenye ulemavu wa macho kutambua thamani ya noti kwa kuipapasa.
Ametoa maelezo mengine ya kiusalama kuwa ni pamoja na Spark R, alama maalum yenye picha ya Twiga inayoonekana kama rangi ya dhahabu inayobadilika kuwa kijani na kurejea dhahabu noti inapogeuzwa, kwa noti za Sh 10,000, 5,000 na 2,000.
Vilevile kuna Lift Twin, alama inayoonesha tarakimu ya thamani na kichwa cha Twiga inapoangaliwa kwa usawa wa macho kwenye noti ya Sh 1,000.
Kwa upande wa kamba ya usalama (security thread),Mwakabalula amesema kuwa sasa imeboreshwa zaidi kwa kuonesha mwanga unaotembea na kubadilika rangi ya pinki kwenda kijani kwa Sh 10,000; bluu kwenda zambarau kwa Sh 5,000; na dhahabu kwenda kijani kwa Sh 2,000 noti inapogeuzwa juu chini au kushoto kulia.

“Unapoielekeza noti kwenye mwanga, kamba hiyo huonesha maandishi kama BOT 10000, BOT 5000 au BOT 2000 kutegemea thamani ya noti husika,zipo alama za wino maalum (UV ink) zinazong’ara katika mwanga wa zambarau kwenye noti za Sh 10,000, 5,000 na 2,000,” amesema.
Mbali na hayo amebainisha kuwa kuzijua na kuzitumia alama hizi kunawasaidia wananchi kuepuka kudanganywa na noti bandia ambazo mara nyingi huonekana kuwa na makosa madogo yasiyoendana na viwango vya utengenezaji wa noti halisi.
Ametumia nafasi hiyo kuwahimiza waandishi wa habari, kutumia majukwaa yao kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua alama za usalama na kutunza fedha kwa usahihi, kwa kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya taasisi za fedha na wananchi.
“Sambazeni taarifa zinazolenga kuinua uelewa wa wananchi ili kusaidia juhudi za Serikali kulinda thamani ya sarafu na kupunguza gharama zisizo za lazima katika uchapishaji wa fedha mpya, ” amesisitiza.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, utengenezaji au usambazaji wa noti bandia ni kosa la jinai linaloangukia chini ya makosa ya uhujumu uchumi na kughushi ambapo mtu yeyote anayekamatwa akitengeneza, kusambaza au kuhifadhi noti bandia kwa kujua, huchukuliwa kama mtuhumiwa wa makosa yanayoathiri uchumi wa nchi.



