📌 Majimbo 7 kati ya 9 yapita bila kupingwa
📌 Kata 92 kati ya 122 zapita bila kupingwa
📌 Maelfu wakusanyika kusikiliza Ilani ya CCM 2025-2030
📌 Dkt. Biteko awasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan
📌 Asisitiza mshikamano kabla na baada ya uchaguzi
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita leo Septemba 2, 2025 kimezindua kwa kishindo kampeni za kuinadi Ilani ya CCM 2025-2030 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo imeelezwa kuwa mpaka sasa tayari Majimbo 7 kati ya 9 ya Ubunge yamepita bila kupingwa huku kata 92 kati ya 122 zikipita bila kupingwa.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe, Mkoani Geita ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa huo, Nicholaus Kasendamila amesema Chama cha Mapinduzi kinaingia kwenye kampeni kikiwa na mtaji mkubwa wa uadilifu, uaminifu, uchapakazi na busara ya mgombea Urais wa kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema kupitia kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, CCM inazo sababu za kuomba ridhaa ya wananchi kuendelea kuongoza nchi akisema kuwa amefanya maendeleo mengi ikiwemo uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kubwa la biashara kwaTanzania na nchi jirani, amejenga daraja refu la Busisi, amekamilisha ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere (MW 2,115) na reli ya kisasa imeshaanza kufanya kazi.
Kasendamila amesema kuwa katika Mkoa wa Geita, Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 imetekelezwa kwa mafanikio ambapo ameeleza kuwa shule mpya za msingi 151 zimejengwa, Shule za sekondari mpya 118 zimejengwa, zimejengwa hospitali mbili za rufaa, hospitali za wilaya mpya 4 na vituo vya afya 17 vipya vimejengwa.
Ameongeza kuwa, kupitia Ilani ya CCM 2020-2025, zahanati 69 zimejengwa, leseni za madini 7600 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo na kuhusu umeme, kabla ya kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Sita kulikuwa na vijiji 362 tu vyenye umeme lakini sasa vijiji vyote 486 mkoani Geita vina umeme.

Kuhusu miundombinu ya Barabara amesema Barabara za lami na changarawe zimeendelea kujengwa mkoani Geita ili kurahisisha usafiri wa wananchi.
Ametaja vipaumbele vya CCM katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuwa ni pamoja na kuongeza fursa za wananchi kujiimarisha kiuchumi, kuendeleza sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, madini, umeme n.k
Mwenyekiti huyo wa CCM, ameomba wananchi waipigie kura CCM kwani kura zao zitafanyiwa kazi kupitia maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Wagombea nafasi ya Ubunge mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye ni Mbunge Mteule wa Jimbo la Bukombe, amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa kampeni akieleza kuwa ni ishara ya Wananchi kukipenda Chama cha Mapinduzi na kuridhika na kazi zinazofanywa na Dkt. Samia suluhu Hassan.

Amesema uchaguzi wa mwaka huu utapeleka salaam ndani ya nchi na kimataifa kuhusu uwepo wa demokrasia nchini hivyo amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura akiahidi kuwa maendeleo wanayoyaona sasa ni rasharasha tu kwani maendeleo makubwa zaidi yanakuja.
Amesema Mkoa wa Geita unazidi kukua ambapo kwa sasa umekuwa ni moja ya mikoa mitano yenye uchumi mkubwa nchini ni mkoa namba moja kwa kuzalisha dhahabu, umekuwa ni mkoa kiungo kwa maeneo mengine nchini na watu wake ni wachapakazi hivyo watampigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kupata maendeleo zaidi.
Kuelekea uchaguzi Mkuu 2025, Dkt. Bitelo amesisitiza kuwa uchaguzi huo uunganishe wananchi badala ya kutenganisha, kuwe na kampeni za kistaarab na Chama cha Mapinduzi kuendelea kufanya kazi kwa umoja.
“Uchaguzi huu ni kwa ajili ya maendeleo yetu, tunataka barabara bora, umeme, afya, mitaji ya biashara, tusiuchukulie poa uchaguzi huu kwani maana kubwa kwenye maisha yetu,” Amesisitiza Dkt.Biteko.

Akizungumzia maendeleo mbalimbali yaliyofanywa katika Jimbo la Bukombe, Dkt. Biteko amesema, chini ya uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan Bukombe sasa kunajengwa Chuo cha VETA ambacho kitawezesha vijana kupata ujuzi wa aina mbalimbali pia Chuo cha Uhasibu Arusha kimeanzisha tawi wilayani Bukombe.
Ameongeza kuwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezigusa sekta zote kimaendeleo akitolea mfano Shule za msingi sasa zimefikia 104, shule za sekondari zimefikia 25 na shule za sekondari kidato cha tano na sita zimefikia 5 huku umeme ukifika kwenye vijiji vyote.
Ameongeza kuwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha ujenzi wa kituo kikubwa cha kuzalisha umeme wa jua wa megawati 5 wilayani Bukombe, kikiwa ni cha pili kwa ukubwa ukiacha kituo cha namna hiyo kilichopo Kigoma pia anajenga barabara ya lami kutoka Ushirombo hadi Katoro.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea mgombea mwenza wa Kiti cha Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye anatarajiwa kuanza ziara mkoani Geita tarehe 5 Septemba 2025.

Awali, Katibu wa CCM Mkoa wa Geita, Alexandarina Katabi amesema Mkoa wa Geita una mtaji wa wapiga kura waliojiandikisha takriban 1,532,408 huku Wanaccm waliojiandikisha wakiwa ni 524,000 ikiwa ni mtaji wa nusu ya wananchi waliojiandikisha.
Amesema katika Mkoa wa Geita, Majimbo yanayogombewa ni 9 na kata ni 122.
Ameongeza kuwa katika Majimbo hayo 9 majimbo 7 tayari yamepita bila kupingwa na katika kata 122 tayari kata 92 zimepita bila kupingwa na zilizobaki ndizo zenye wapinzani.

