Mbio za Urais 2025: Vyama 17 Vyaidhinishwa, ACT Wazalendo Nje

Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo Agosti 27, 2025, imetangaza orodha ya wagombea wa urais watakaoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo jumla ya vyama 17 pekee ndivyo vilivyopitishwa rasmi.

Chama cha ACT Wazalendo hakijajumuishwa, hali inayomwondoa rasmi mgombea wao, Luhaga Mpina, katika kinyang’anyiro hicho.

Kupitia ubao wa matangazo wa ofisi za INEC jijini Dodoma,umeonyesha kuwa ACT Wazalendo ni miongoni mwa vyama vilivyoshindwa kufikia vigezo vya tume hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa INEC, Kailima Ramadhan, amesema kuwa vyama vilivyopitishwa vimekidhi masharti yote muhimu kwa mujibu wa sheria na taratibu za uchaguzi.

Kampeni za wagombea hao sasa zitaanza rasmi kesho, Agosti 28.

Uamuzi wa kutokupitishwa kwa ACT Wazalendo unaibua maswali kuhusu hatma ya ushiriki wa chama hicho katika uchaguzi mkuu, hasa ikizingatiwa kuwa kimekuwa kati ya vyama vinavyotoa upinzani mkubwa katika siasa za Tanzania kwa miaka ya karibuni.