Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Subira Mgalu, atembelea miradi ya maendeleo 35 akijionea hatua za utekelezaji na changamoto zilizopo, huku akichangia milioni 15 kwa ajili ya kuimarisha miradi ya nguvu za wananchi.
Ziara hiyo ni ya awali ya shukrani aliyofanya Mbunge huyo katika kata Jimbo la Bagamoyo, akiwashukuru wananchi kwa imani waliyoionesha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kupitia ziara hiyo, Mgalu amechangia sh. milioni 15 kwa ajili ya kukamilisha na kuimarisha miradi ya nguvu za wananchi, ikiwemo milioni moja ujenzi wa uzio shule ya msingi Mwanamakuka na 500,000 kwa umoja wa vijana bodaboda Gate No. 1 kata ya Dunda.
Akizungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali aliyotembelea, aliwahakikishia kuwa ataendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Chama na Serikali ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kwa haki, uwazi na usawa.
Vilevile Mgalu alihamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuanza utekelezaji wa mpango huo kwa kuzingatia makundi maalum ikiwemo wazee, watu wenye ulemavu, wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Aidha, alivitaka vyama vya siasa, viongozi wa Serikali na wadau kuwa na umoja ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa na hivyo kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma za afya kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali kupitia Wizara ya Afya.
Ziara hiyo imehusisha mikutano saba (7) ya ndani iliyowakutanisha wajumbe wa Kamati za Siasa za Kata, Sekretarieti za Chama, viongozi wa vijiji na vitongoji na watendaji wa Serikali ambapo amefanya na mikutano tisa (9) ya hadhara.


