Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MCHEZAJI wa kulipwa kutoka Gymkhana Dar es Salaam, Fadhil Nkya ameibuka mshindi kwa mara ya sita mfululizo katika mashindano ya gofu ya Lina PG Tour yaliyomalizika jana na kujinyakulia kitita cha Shilingi milioni 6.8.

MASHINDANO hayo ya gofu ambayo kumuenzi nyota wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake, marehemu Lina Nkya, yalianza Julai 17, 2025 katika Viwanja vya Lugalo, jijini Dar es Salaam, huku wachezaji 150 kutoka kona mbalimbali za nchi wakishiriki.

Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Fadhil alieleza kuwa mashindano yameboreshwa na yalikuwa ya ushindani mkubwa.

“Kadri siku zinavyoenda ndo mashindano yanazidi kuwa mazuri. Hivyo niwasihi na wachezaji wenzangu waweze kupambana na kuongeza bidii katika mchezo huu,” amesema.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kuyapa nguvu zaidi mashindano hayo kwa kuhakikisha kunapatikana wafadhili wengi zaidi, ili hatimaye kusaidia kuunda timu ya taifa ya gofu itakayowakilisha nchi kimataifa.

Kwa upande wake, Christina Charles kutoka Morogoro Gymkhana alisema licha ya kutofanya vizuri, ameona thamani ya ushiriki wake na kujifunza mengi kwa ajili ya msimu ujao.

“Nashukuru Lina PG Tour kwa kusapoti mashindano haya. Sijafanya vizuri sana lakini nimejifunza. Wachezaji wenzangu nawahamasisha waongeze juhudi kwenye mazoezi,” alisema Christina.

Naye Saidi Nkya, mmoja wa waanzilishi wa mashindano hayo, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa Lina PG Tour kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wachezaji wa kulipwa (maPRO), huku idadi yao ikizidi kuongezeka.

“Tumeanza na wachezaji wachache, lakini sasa wameongezeka hadi kufikia 25, na waliocheza uwanjani walikuwa 22. Kutokana na mafanikio haya, tunategemea kuanzisha mashindano maalum kwa watoto yanayoitwa Lina Junior Tour kwa lengo la kulea vipaji,” alieleza Nkya.

Ameongeza kuwa watoto watakaofanya vizuri kwenye Junior Tour watachukuliwa na kushiriki mashindano makubwa ili kupata uzoefu, huku watano bora wakipewa fursa zaidi.

Katika kutanua wigo wa mashindano, Nkya alisema kuwa mwaka ujao wanapanga kuyasogeza mashindano haya hadi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ikiwa ni juhudi za kuongeza wachezaji wa kulipwa na hadhi ya mashindano.

Naye Nahodha wa klabu ya gofu ya TPDF Lugalo, Meja Japhet Masai aliwapongeza waandaaji wa mashindano ya Lina PG Tour ambapo amesema mashindano hayo yamefanyika vizuri na kutoa fursa kwa wachezaji kutoka sehemu mbalimbali nchini kushiriki.

Alisema pamoja na michuano hiyo kufanyika vizuri aliwaomba wachezaji wa gofu kuendelea kudumisha upendo na mshikamano ili kuhakikisha mchezo huo unazidi kukua na kuimarika nchini.

“Watu wamejitokeza kwa wingi na tumejifunza mambo mengi hasa ushirikiano ulioneshwa, tumeshuhudia uimara wa uwanja wa Lugalo hivyo tunawapongeza wale wote walioshinda na kuwataka ambao hawakushinda kujipanga upya na mashindano yajayo,” alisema Meja Masai

Kwa upande wa wachezaji chipukizi (Elites), Prosper Emmanuel aliibuka mshindi na kujinyakulia Shilingi milioni 2.2, huku Julius Mwinzani na Gabriel Abel wakifungana nafasi ya pili, kila mmoja akijipatia Shilingi milioni 1.1.

Mashindano haya yanatajwa kuwa sehemu muhimu ya ukuzaji wa mchezo wa gofu nchini, hasa kwa vijana, wanawake, na wachezaji wanaochipukia.