Na Zulfa Mfinanga JamhuriMedia, Arusha

Katika kuelekea kipindi nyeti cha uchaguzi Mkuu nchini, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa mwongozo muhimu kwa wanahabari, vyombo vya habari, taasisi za kiraia, vyuo vya uandishi wa habari, na makundi mengine likisisitiza utii wa maadili ya taaluma na kuondoa uwezekano wa migongano ya kimaslahi.

Mwongozo huo umesomwa leo na Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza hilo, Ernest Sungura, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha.

Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), Ernest Sungura.

Amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki kwa kila raia ikiwemo waandishi wa habari kushiriki katika mchakato wa kugombea nafasi za kisiasa, hata hivyo amesisitiza kuwa wanahabari wote wanaonuia kushiriki siasa lazima wajiondoe mara moja kwenye vyumba vya habari ili kulinda hadhi, uaminifu na uhuru wa tasnia ya habari.

“Kuendelea kuwa mwandishi wa habari huku ukigombea nafasi ya uongozi ni kinyume cha maadili ya taaluma, lazima ujiondoe ili kuepusha mgongano wa maslahi na kupoteza uaminifu wa umma,” alisema Sungura kwa msisitizo.

Ameeleza kuwa wanahabari wanaojihusisha na siasa wakiwa bado wanaripoti wanaiweka tasnia kwenye hatari ya kutumiwa kama chombo cha propaganda jambo linalodhoofisha hadhi ya vyombo vya habari na kuondoa imani ya wananchi kwa taarifa zinazotolewa.

Sungura amesema hali hiyo inaweza kusababisha taarifa zenye upendeleo au ajenda binafsi.

Baraza pia limetoa angalizo kwa vyombo vya habari vinavyoegemea upande fulani wa kisiasa kuhakikisha vinazingatia mizania, usahihi na weledi katika uandishi wa habari na kwamba havipaswi kutumiwa kama jukwaa la kushambulia vyama pinzani au viongozi wa upande mwingine.

“Chombo cha habari kinaweza kujitambulisha na mlengo wa kisiasa, lakini hakiwezi kupewa ruhusa ya kukandamiza sauti za vyama vingine,” alifafanua Sungura na kuongeza kuwa uhuru wa habari hauwezi kutenganishwa na uwajibikaji kwa jamii nzima.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, taasisi za kiraia na za habari zimetakiwa kuhakikisha zinazingatia dira na dhima zao hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kutoa elimu sahihi kwa umma na kusaidia kulinda uhuru wa vyombo vya habari dhidi ya upotoshaji au ushawishi wa kisiasa.

Aidha vyuo vya uandishi wa habari vimetakiwa kubuni kozi maalum kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi ambapo mafunzo hayo yanatakiwa kujikita katika sheria, maadili, na miiko ya uchaguzi ili kusaidia wanahabari kuandika taarifa zenye mizania na kulinda amani ya Taifa.

Katika hatua nyingine MCT imekumbusha umuhimu wa Azimio la Dar es Salaam juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji (DEFIR) likieleza kuwa azimio hilo linaweka msingi wa maadili kwa makundi yote yanayohusika na uchaguzi wakiwemo wanasiasa, wamiliki wa vyombo vya habari, wafadhili, na jamii kwa ujumla.

Sungura amewataka wamiliki na wakurugenzi wa vyombo vya habari kutoingilia maamuzi ya wahariri na wanahabari kwa misingi ya maslahi ya kisiasa au kibiashara kwani kufanya hivyo kunaathiri uhuru na uaminifu wa vyombo hivyo kwa wananchi.

Aidha ameonya kuwa watangazaji na wafadhili hawapaswi kutumia nguvu zao kiuchumi kushinikiza mwelekeo wa taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari bali waheshimu uhuru wa uhariri na ajenda ya kitaifa inayolenga ustawi wa umma.

Kwa upande wa jamii MCT imehimiza wananchi kuwa na mwamko wa kuzitathmini taarifa wanazopokea, kutoa mrejesho kwa wahariri na kuwa sehemu ya mchakato wa kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi bila upendeleo wa kisiasa.

Mwongozo huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu huku Baraza la Habari Tanzania likionya dhidi ya matumizi mabaya ya vyombo vya habari na kushawishi mazingira ya chuki, upotoshaji au propaganda zisizo na mizania.

Amesema Baraza litaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa vyombo vya habari na wanahabari katika kipindi chote cha uchaguzi ilu kuhakikisha kuwa taaluma hiyo inatumika kwa manufaa ya taifa na si kwa faida ya kikundi au mtu binafsi.

Mwongozo huo unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu kwa kila mdau wa habari nchini katika kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki, na wa amani unawezekana kupitia taarifa sahihi, zenye mizania na zinazozingatia maadili ya uandishi wa habari.