…………………………

Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Ladislaus Mnyone, amesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu ni nguzo muhimu ya kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.

Prof. Mnyone aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa kufundishia na kujifunza ulioratibiwa na Raoma Foundation kupitia kampeni ya Twenzetu Darasani, unaowezeshwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania.

Alisema Mheshimiwa Ameir alitamani kuhudhuria binafsi kuzindua mfumo huo, lakini kutokana na majukumu mengine ya kikazi alimuelekeza yeye kumwakilisha katika tukio hilo muhimu kwa taifa.

“Teknolojia hii itasaidia kuongeza fursa za elimu na wakati huo huo kuboresha ubora wa elimu nchini. Ni jibu la changamoto ya uhaba wa walimu na tofauti ya viwango vya ufundishaji kati ya maeneo,” alisema Prof. Mnyone.

Alieleza kuwa juhudi hizo zinaendana moja kwa moja na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13 alisisitiza umuhimu wa kuziunganisha shule zote nchini kwa mifumo ya kidijitali ili watoto wapate elimu bora bila kujali walipo.

Akizungumzia Dira ya Maendeleo 2050, Prof. Mnyone alisema taifa linakusudia kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, kuongeza pato la mtu mmoja mmoja hadi dola za Marekani kati ya 7,000 na 12,000, pamoja na kuhakikisha zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wanakuwa na ajira zenye staha.

“Malengo haya hayawezi kufikiwa bila kuwa na rasilimali watu yenye maarifa na ujuzi wa kutosha. Elimu bora na matumizi sahihi ya teknolojia ni silaha muhimu ya kufanikisha hilo,” alisisitiza.

Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, pamoja na mitaala iliyoboreshwa ili kuendana na mahitaji ya sasa.

Alitaja miongoni mwa mageuzi hayo kuwa ni upanuzi wa elimu ya lazima kutoka miaka saba hadi kumi, pamoja na kuanzishwa kwa mkondo wa elimu ya amali unaolenga kuwajengea wanafunzi stadi za vitendo mapema.

Prof. Mnyone alisema ongezeko la wanafunzi na mabadiliko ya sera yameongeza mahitaji ya miundombinu, walimu na vifaa, hali inayofanya matumizi ya teknolojia kuwa suluhisho muhimu la kusaidia mwalimu mmoja kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

“Lengo si tu kuwafanya vijana wawe watumiaji wa teknolojia, bali wawe wabunifu na wazalishaji wa teknolojia hizo,” aliongeza.

Kwa upande wake, uongozi wa Raoma Foundation ulieleza kuwa mfu

mo huo wa kidijitali utawezesha utoaji wa elimu kwa usawa nchini na kusaidia kuharakisha utekelezaji wa maono ya serikali katika sekta ya elimu.