Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Nyambi Athuman ambaye ni mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), ambapo CUF inaamini katika falsafa ya ‘Haki Sawa kwa Wote’ itahakikisha kila mwananchi anapata haki zake za kiuchumi, kijamii, mazingira bora na kipato cha msingi endapo wataichagua.

Akizungumza wakati wa kampeni katika mkutano uzunduzi wa kampeni uliofanyika eneo la Soko la Mawenzi, Manispaa ya Morogoro juzi alisema kuwa endapo watamchangua kuwa mbunge wao atasimamia utekelezaji wa Ilani ya chama chake yenye maeneo 13 ya vipaumbele.

“Ichagueni CUF ili tutekeleze falsa yetu ya ‘Haki Sawa kwa Wote’ Pamoja na kutekeleza ilani ya chama yenye maeneo 13 ili wananchi mjiimrishe kiuchumi” alisema.

Athumani liyataja maeneo hayo ya vipaumbele ni pamoja na uboreshaji wa huduma za maji, elimu, afya, na miundombinu ambayo ni maono ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ifikapo mwaka 2030.

Alisema katika ilani hiyo imeelekeza kuboresha afya njema hususani kwa akina mama wajawazito na watoto kwa kupatiwa huduma bure, ustawi wa jamii, elimu bora kuanzia awali hadi chuo kikuu na jumuishi, kusimamia usawa wa kijinsia na haki za kundi maalumu.

Alisema endapo atachaguliwa atahakikisha anasimamia ilani hiyo ambayo imeelekeza hatua mbalimbali zikiwemo za kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira.

Alitaja maeneo ya vipaumbele katika ilani hiyo ni kutokomeza umasikini kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya uzalishaji mali, SACCOS na huduma jumuishi za kifedha.

Pia, kupanua ajira nadhifu kupitia programu za kilimo, biashara ndogo za kazi na viwanda vidogo na kuanzisha mpango wa ruzuku ya huduma za msingi kwa familia masikini.