Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Kagera

Zikiwa zimesalia siku chache wananchi kutimiza haki na wajibu wao wakuwachagua viongozi wa udiwani, wabunge na Rais mgombea udiwani kata Mabale Jimbo la Misenyi mkoani Kagera kupitia tiketi ya ACT WAZALENDO Mhandisi Sweetbert Kaizilege John ameendelea kuchanja mbuga na kutumia nafasi vizuri kwakuwafikia wananchi akiwahidi kuwajibika ipasavyo katika kuyatekeleza mambo mbalimbali ya maendeleo ndani ya kata hiyo.

Mgombea Sweetbert akiwahutubia wananchi wa kitongoji cha Kigarama kijiji Nyankele katika mwendelezo wa kampeni zake kuelekea uchaguzi ameendelea kuzimwaga sera mbalimbali kwa wananchi.

Akiwa hapo Kigarama amevitaja baadhi ya vipaumbele atakavyoanza navyo ni pamoja na kutatua kero ya maji ambayo ni changamoto kubwa maeneo mengi ya kata, barabara, afya, elimu pamoja na bima ya afya kwa wazee.

Mbali na hayo amewahakikishia wananchi kuwa dhamira yake ni kuiona Mabale inabadilika na kupiga hatua mbele kimaendeleo kuliko ilivyo kwa sasa.

Hata hivyo amesema anatamani kuiongoza Mabale yenye umoja, upendo, mshikamano maelewano rika zote sambamba na kuboresha ushiriano kwa watumishi wa idara tofauti tofauti wanaowatumikia wananchi wakiwemo walimu, wahudumu wa afya na wengineo.

Mhandisi Sweetbert ameongeza kuwa atakapochaguliwa pia atakutana na kundi la vijana ili kuzitatua changamoto zinazo wakabili hasahasa kuinua sekta ya michezo kama walivyokwisha toa ombi hilo kwake hivyo amewaomba wananchi kumchagua kwa kishindo ili aweze kuitimiza adhima yake ya kuwaletea maendeleo.

Mgombea udiwani Sweetbert Kaizilege

Mikutano ya kampeni za mgombea huyo imejikita kuwafikia wananchi kitongoji kwa kitongoji ikiendelea kuwavutia wananchi walio wengi kutokana na ahadi zake zenye maendeleo ya kumgusa kila mmoja huku wakifurahishwa na mfumo anaoutumia katika mikutano hiyo wa kuwatengea nafasi ya kuwasikiliza changamo zao naye akiwaahidi moja kwa moja kuzishughulikia baada ya kumchagua Tarehe 29, Oktoba 2025.

Naye katibu wa chama jimbo la Misenyi, Laulian Kabakama akiwa bega kwa bega na wagombea udiwani kata za Mabale, Kilimilile, Kyaka na Bugandika amewahakikishia wananchi wa Kigarama kuwa chama hakijakosea kuwateua wagombea hao shupavu akiwemo Sweetbert Kaizilege John, chama kimewakubali na kuwaamini hivyo wananchi wasifanye makosa yakutokuwachagua ili wayashuhudie mabadiliko makubwa ya maendeleo chini ya ACT WAZALENDO.

Katibu wa chama Jimbo Misenyi Lauliani Kabakama.