Mgombea udiwani kata ya Mabale jimbo la Missenyi mkoani Kagera kupitia ACT WAZALENDO Sweetbert Kaizilege John ameahidi kujenga kituo kipya cha kutolea huduma ya kliniki kwa watoto kitongoji Nyamilembe kijiji cha Kibeo ili kuwanusuru na changamoto wanazokabiliana nazo akina mama na watoto wanaotumia kituo kilichojengwa kwa nguvu ya wananchi kutokana na kituo hicho kuwa katika hali mbaya ya kuchakaa.

Mhandisi Sweetbert ametoa kauli hiyo akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni zake uliofanyika eneo ilipo zahanati hiyo na kusema kuwa hali ya jengo hilo ni hatarishi kwa matumizi kutokana na kuta zake zilizokandikwa kwa udongo kupoteza uimara na kuendelea kubomoka hatimaye kubakia miti pekee.

Amesema iwapo atachaguliwa tarehe 29 Oktoba, 2025 mapema ataanza ujenzi mara moja kabla ya mambo mengine kutokana na uhitaji wa kituo hicho kwa wananchi.

Hata hivyo amewahakikishia wananchi kwamba iwapo watampatia nafasi yakuwatumikia atatatua changamoto ya maji, barabara na ajira kwa vijana wa kata hiyo.