Mgombea Urais wa Colombia, Miguel Uribe, amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumanne, miezi miwili baada ya kushambuliwa kwa risasi alipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi.

Licha ya kuonyesha dalili za kupona katika wiki za hivi karibuni, madaktari walibainisha kuwa mwanasiasa huyo alianza kuvuja damu kwenye ubongo siku ya Jumamosi, hali iliyosababisha kifo chake.

Uribe, aliyekuwa na umri wa miaka 39 na Seneta wa chama cha kihafidhina, alipigwa risasi kichwani na mguuni Juni 7, 2025, wakati akihutubia mkutano wa hadhara jijini Bogota.

Jeshi la polisi limesema watu sita wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo, akiwemo mshambuliaji kijana mwenye umri wa miaka 15. SOMA: Mahakama yamkuta Uribe na hatia

Kifo cha Uribe, ambaye alitarajiwa kupambana na Rais Gustavo Petro katika uchaguzi wa mwaka ujao, kimezua hofu ya kurejea kwa Colombia katika wimbi la ghasia za kisiasa.