Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
CHAMA Cha Democratic Party (DP) kimezindua mikutano yake ya kampeni za Urais, Ubunge na udiwani katika uwanja wa stendi ya zamani Mjini Tabora na kuahidi kuboresha mafao ya wastaafu nchini.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika jana mjini hapa, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho Abdul Juma Mluya amesema kuwa akipewa ridhaa kuwa rais wa Tanzania atamaliza kero za wastaafu.
Amebainisha kuwa serikali itakayoundwa na chama chake itafuta kikokotoo kinachotumika sasa kulipia wastaafu kwa sababu hakiwasaidii bali kinawaongezea presha ya maisha na kusababisha wafe mapema.

‘Falsafa ya DP ni kulinda haki, usawa na maslahi ya wananchi, hivyo kama watapewa ridhaa ya kushika dola Oktoba 29 mwaka huu, ndani ya siku 100 za kwanza atakomesha dhuluma zote kwa wananchi ikiwemo wastaafu’, amesema.
Mluya ameongeza kuwa serikali ya chama chake itawakopesha nyumba watumishi wote ili wale watakaostaafu wasihangaike bali wawe na mahala pa kuishi na wale watakaoshindwa kulipa mikopo ya nyumba zao watalipa kupitia mafao yao.
‘Serikali ya Chama Cha Democratic Party itawaheshimisha watumishi wote wakiwemo maaskari kwa kuwapa mishahara mizuri ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi mkubwa’, ameongeza.
Mluya ametaja vipaumbele vingine vilivyoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama chake kuwa ni kuruhusu uraia pacha kwa diaspora wote ili kuwapa fursa ya kuja kuwekeza nchini, kufumua mikataba ya madini yote na kuanza upya.

Vingine ni kusimamia ipasavyo rasilimali za nchi ili zinufaishe wazawa na kudhibiti utoroshaji malighafi nje ya nchi, pia serikali yake itatunga sheria itakayowabana watoto ili watakapokua wakubwa watunze wazazi wao.
Aidha watadhibiti wanunuzi wanaoibia wakulima, watajenga kiwanda cha asali Tabora, kiwanda cha tumbaku kitahamishwa kutoka Morogoro kuja Tabora, wajawazito watajifungua bure na watapiga marufuku hospitali zote kutoza maiti.
Naye Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama hicho Saadun Abdulrahman Khatibu amesisitiza kuwa chama cha DP kipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi hivyo akawaomba wawapigie kura za kutosha ili washike dola.


