Mamilioi ya watu wanajiandaa kwa wiki ya changamoto ya usafiri jijini London Uingereza kutokana na mgomo wa treni za chini kwa chini.

Mamilioni ya watu wanajiandaa kwa wiki ya hekaheka na matatizo ya usafiri jijini London Uingereza huku wafanyakazi wa treni za chini ya ardhi jijini humo wakianza mgomo wa siku tano.

Mgomo huo ulioanza jana Jumapili umesababisha vituo vya treni kufungwa na kutishia kulemaza mfumo mzima wa usafiri.

Njia kadhaa za reli katika mtandao wa usafiri wa chini ya ardhi hazikufanya kazi jana jioni na shirika linalosimamia mfumo wa usafifi jijini London, TfL, limesema kutakuwa na huduma chache ama kusiwe na huduma zozote leo Jumatatu na siku ya Alhamisi.

Chama cha wafanyakazi cha RMT kimeitisha mgomo huo wa mfumo wa treni za chini ya ardhi unaotumiwa na abiria milioni tano kwa siku, huku kikipambana kupata makubaliano ya mishahara mizuri zaidi na mazingira bora ya kufanya kazi.

Madereva watafanya mgomo pamoja na wafanyakazi wanaofanya matengenezo baada ya kukataa mapendekezo ya nyongeza ya mshahara ya asilimia 3.4 yaliyopendekezwa na shirika la TfL.