Na Stella Aron, JamhuriMedia, Tanga

Mikoko ni moyo wa uchumi wa buluu. Bila mikoko,mazingira baharini yangekuwa dhaifu, maisha ya viumbe wa pwani yangepungua na uchumi wa jaii za pwani ungeathirika.

Pamoja na faida hizo baadhi ya watu hukata mikoko kwa kuni, mbao vitendo ambavyo hupunguza kasi ya ukuaji wa mikoko na kuharibu mazingira ya baharini.

Tunaweza kusema kuwa mikoko ni muhimu sana lakini inakumbwa na hatari kubwa hivyo nguvu ya pamoja na inahitaji kushirikiana na jamii, Serikali na wadau wengine kuitunza kwa ajili ya mazingira bora na uchumi edelevu wa bahari.

Katika muktadha wa kukuza uchumi wa buluu nchini Tanzania, mikoko imeendelea kuonekana kama rasilimali ya kimkakati inayochangia maendeleo endelevu ya jamii za pwani. Mikoko ni miti ya pekee inayoota kwenye maeneo ya maji ya chumvi, hususan kwenye pwani, mito na maeneo ya baharini.

Kuna faida nyingi zitokanazo na miti ya mikoko lakini baadhi ya wananchi hawana uelewa juu ya faida hizo, ili kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira jamii inahitaji elimu zaidi ambapo mikoko hutoa makazi kwa viumbe mbalimbali wa baharini kama samaki, kaa, na kamba. Hii huongeza mazao ya uvuvi ambayo ni chanzo muhimu cha chakula na kipato kwa familia nyingi.

Pia, mikoko huimarisha usalama wa pwani kwa kuzuia mmomonyoko wa ardhi na mafuriko yanayosababishwa na mawimbi makubwa ya bahari na ni kivutio kikubwa cha utalii wa mazingira (eco-tourism), ambapo wageni kutoka ndani na nje ya nchi hufika kujionea mandhari ya kipekee ya misitu ya mikoko. Hii huongeza mapato na ajira kwa jamii. Mikoko huchangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza hewa ukaa kwa kiwango kikubwa.

Ili kupata mafanikio chanya kasi ya juhudi za kukuza uchumi wa buluu wananchi wanapaswa kupata elimu ya faida za utunzaji mikoko, upandaji wa mikoko mipya, kutoa elimu kwa jamii, na kusimamia sheria za mazingira ni muhimu kwa uhifadhi wa mikoko.

HEKARI 9.6 ZA MIKOKO ZAREJESHWA

Meneja wa Mpango wa Ustahimilivu wa Pwani na Bahari wa Taasisi ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Joseph Olilla Joseph Olila, anasema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo hekari 90.6 za mikoko zimerudishwa katika hali yake ya asili katika mwambao wa Bahari ya Hindi unaopita Tanga katika Tanzania Bara na Pemba katika Visiwa vya Zanzibar.

“Kuna maeneo wananchi wamepata elimu ya masuala ya uhifadhi wa mazingira ya Bahari na kurejeshwa uoto wa asili wa miti ya mikoko ndani ya miaka mitatu na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu matarajio yetu ni kufikia hekta 100″ anasema.

Olila anasema kuwa kupitia mradi wa Bahari Mali uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya
ufadhili wa Ubalozi wa Ireland kwa kutoa elimu kwa jamii ikiwa ni pamoja na urejeshaji wa miti ya mikoko katika eneo la Tanga kwa Wilaya ya Mkinga, Pangani na Pemba kwa wilaya mbili za Mkoani na Micheweni.

“Kazi ya kurejesha mikoko si rahisi, na kufanikisha zaidi ya hekari 90 ni mafanikio makubwa yanayopaswa kuthaminiwa.Watu wamekuwa wakikata mikoko kwa matumizi mbalimbali kama kuni, utengenezaji wa mitumbwi na ujenzi wa nyumba na kusababisha uharibiu mkubwa” anasema.

Tanzania ina zaidi ya kilomita 1400 za mwambao wa Bahari ya Hindi, lakini bado, hasa bara, haijafaidika ipasavyo na uchumi wa buluu.

“Kwa kiwango kikubwa, watu wa Zanzibar wameweza kutumia rasilimali za bahari kujipatia kipato na kukuza uchumi wa visiwa. Kwa sasa wameweza kunufaika na uchumi wa buluu kwa zaidi ya asilimia 80,” anabainisha.

Akizunguza waandishi wa habari za mazingira kutoka Chama cha Waandishi wa Habari wa Mazingira Tanzania (JET), mkoani Tanga katika warsha maalum ya mafunzo kuhusu Uchumi wa Buluu iliyoandaliwa na IUCN, anasema kuwa urejeshaji wa mikoko siyo tu kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuzuia mmomonyoko, bali pia umeleta fursa za kiuchumi kwa jamii za pwani.

“Kwa sasa watu wanaanza kuvuna asali ya mikoko, aina mpya ya asali tamu ambayo inapata soko kubwa ndani na nje ya nchi,” anasema.

BAHARI KUATHIRIWA

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dk Rushingisha George anasema kuwa katika utafiti wao kuhusu Mradi wa Mali Bahari umeoneshakuwa na matokeo mazuri.

“TAFIRI kwenye Mradi wa Mali Bahari tumekuwa tukiangalia kipengele cha Asidi Bahari na hali ilionesha bahari yetu imekuwa ikiathirika. Tumetoa taarifa sahihi ambazo zimekuwa zikitumiwa kuidhibiti kwa kutoa elimu na kurejesha hali ya awali,” anasema.

Malengo ya mafunzo na ziara ya mafunzo iliyofanyika baadaye yalikuwa ni kuwawezesha waandishi wa JET kuelewa vizuri zaidi juu ya masuala ya uchumi wa buluu kwa njia ya mafunzo na uzoefu wa moja kwa moja, na kuwapatia ujuzi wa kuhamasisha jamii kufahamu umuhimu wa kutunza mazingira.

“Ndani ya hizo wilaya tunatekeleza shughuli mbalimbali ambazo zimejikita katika kutatua changamoto zilizopo katika uchumi wa buluu kwa kuangalia masuala ya uzalishaji unaofanywa na vikundi vya kijamii kwa mazao ya bahari kama mwani, majongoo bahari, kaa na ufugaji wa samaki,” anasema.

Anasema mradi huo utawawezesha wananchi kujikwamua na umaskini na kufanya shughuli zao ambazo ni endelevu na rafiki kwa mazingira.

Anaongeza kuwa wamekuwa wakiangalia masuala ya uhifadhi na urejeshwaji wa bainuwai kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii kwa kufanya urejeshwaji wa ‘species’ mbalimbali za mikoko.

Wamekuwa wakifanya tafiti kwa kushirikiana na wadau wengine na wamefanikiwa kuangalia eneo la asidi bahari hivyo mradi huo utawasaidia wananchi kutambua fursa zitokanazo na bahari.

“Mpaka sasa tumewafikia wananchi zaidi 400 ambao wamefanikiwa kupitia mradi huu ambao umeleta mabadiliko ya kipato chao. Kwa sasa tunafuatilia hali ilivyo ya utekelezwaji kwa maeneo yaliyorejeshwa uoto huo na matarajio ifikapo mwishoni mwa mwaka huu muda ambao mradi utakuwa unafikia mwisho tuwe tumefikia zaidi ya hekta 100,” anasema.

Anasema kwa sasa bahari inaathiriwa na ongezeko la asidibahari hivyo kuna mbinu za kukabiliana nazo kwa kupata taarifa sahihi, kufanya tafiti kuangalia athari za tatizo, kutoa elimu na kutekeleza mikakati inayoweza kupunguza athari kwa jamii.

Lengo la programu hii ni kuwezesha wananchi kujikwamua kwenye umasikini, kufanya shughuli kwa namna endelevu na rafikikwa mazingira na kuhakikisha uchumi wa buluu unaleta matokeo chanya,” anasema.

“Tumehifadhi na kurejesha baionuwai katika uoto wa asili eneo lenye takribani hekta 904 mkoani Tanga na Pemba. Matarajio hadi mwisho wa mwaka kufikia hekta 100” anasema.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alisema JET imedhamiria kuwa mdau muhimu katika kufanikisha mafanikio ya uchumi wa buluu.

“Sasa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imetoka na kuhimiza masuala ya uchumi wa buluu hivyo tumeona ni fursa kwa waandishi wa habari za mazingira kujifunza na kuujua uchumi wa buluu na namna watakavyoshiriki kuutangaza,” anasema.

KULIKONI KUWA JANGWA LA WACHAWI

Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Joel Mwapagala, anasema eneo hilo liliitwa Jangwa la Wachawi kwa sababu kadhaa.

Anasema kulikuwapo shughuli za kuchimba chumvi miaka ya nyuma miaka ya 1900, hali iliyofanya mikoko kukatwa kwa wingi.

Mwapagala anasema, pia eneo hilo lilikuwa likitumiwa na watu wasio na nia njema kufanya uhalifu na wale waliotafutwa, walikimbilia katika eneo hilo kujificha.

Anasema, baadaye zikawekwa sheria ndogo kupitia sheria mama ya uhifadhi wa mazingira na uhifadhi rasilimali, ilizuia watu kufanya shughuli zozote katika eneo hilo na anayepatikana sheria kali inachukuliwa dhidi yake.

Tathmini iliyofanywa na IUCN mwaka 2024 kwa kutumia mfumo uitwao ‘Red List of Ecosystems’ imebainisha kuwa takriban nusu (asilimia 50) ya mifumo ya ikolojia ya mikoko duniani ziko hatarini kupotea, kutokana na shughuli za kibinadamu.

Tathmini hiyo imeonya, kama hatua madhubuti zisipochukuliwa takribani kilomita za mraba 7,065 za mikoko sawa na asilimia tano zinatarajiwa kutoweka kabisa, huku kilomita za mraba 23,672 sawa na asilimia 16 zitafunikwa na maji kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

USHUHUDA WA VIKUNDI

Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo kilichopo kaika kijiji cha Msarazi Kata ya Bushiri wilayani Pangani, Said Bakari anasema kuwa ujio wa IUCN umeongeza uelewa kwa jamii ambapo katika kikundi chao chenye wanachama 25 na wamejikita katika urejeshaji wa mikoko baada ya kuwezeshwa na IUCN kwa kuwapatia sh milioni 32,000, 000 ambazo zimetumika kujenga mabawa ya samaki, nyavu, kuweka kamera, fensi, teni za mai, mashine ya kujazia maji na bomba za kuingiza maji.

“IUCN wametusaidia kuujua uchumi wa buluu na namna ya kunufaika na ikiwa ni pamoja na kuongeza kazi ya utunzaji mazingira ambapo awali kasi ilikuwa ndogo lakini pia wananachi kuona faida ya mto Pangani ambapo sasa wanajihsisha na kilimo cha kujikimu na si kujishughulisha ha masuala ya bahari mali tu” anasema.

Mwaka 2023, kikundi hicho kilipata ufadhili kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN) na kuandaa mpango kazi wa kurejesha ekari 10 za mikoko katika maeneo ya vitalu vitatu ikiwamo Jangwa la Wachawi.

Anasema kuwa wamesharejesha ekari mbili katika eneo la Jangwa la Wachawi ambalo limeharibiwa sana. ila changamoto ni fedha, na kwamba wao wapo tayari kufanya kazi hiyo iwapo watawezeshwa.

Anasema kuwa Jangwa la wachawi lina maajabu yake kama huna uzoefu na huna ujasiri unaweza kufika mahali ukaamua kusimama katikati ya tope ukisubiri wenyeji wakusaidie kwenda mbele au kurudi nyuma.

Anasema IUCN imewafungua na kutambua kuwa wana jukumu la kutunza mazingira na sio kuwaachia watu kutoka nje ambao hawakuhusika na uharibifu hua.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Ulinzi na Ujasiriamali wa Bahari na Pwani (BMU) kilichopo Pangani Magharibi, Fatuma Mwinyihaji anasema pamoja na upandaji wa miti, pia wanapanda miti mingine ya kivuli kusafisha mitarona kusafisha fukwe.

Pia wamerejesha zaidi ya hekta sita kwenye maeneo mbalimbali likiwemo eneo la Jangwa la Wachawi ambako wamerejesha ekari mbili, Bomba Mbili ekari mbili na Kumba ekari 2 na pia wameotesha miche 5,000.