Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

Halmashauri ya jiji la Arusha imetoa mikopo ya asilimia kumi isiyo na riba ya jumla ya shs bilioni 2.65 kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuinua uchumi wa wananchi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Aprili 9, 2026 Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, amesema kuwa kati ya fedha hizo, vikundi 120 vya wanawake vimepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.632.

Ameongeza kuwa,vikundi 35 vya vijana vimepatiwa shilingi milioni 530.5, huku vikundi 16 vya watu wenye ulemavu vikipokea jumla ya shilingi milioni 102.

“Utoaji wa mikopo hiyo katika awamu hii umeboreshwa kwa kiwango kikubwa, hasa katika vigezo vya upatikanaji wake, jambo lililowezesha wananchi wengi zaidi kunufaika. “amesema Iranghe.

Amefafanua kuwa, moja ya maboresho muhimu ni utoaji wa elimu kwa waombaji wa mikopo hiyo, badala ya mfumo wa awali wa mafunzo ya muda mrefu wa wiki moja hadi sita.

“Mbinu hii imeongeza ufanisi na tija katika matumizi ya mikopo hiyo na imeviwezesha vikundi mbalimbali kuweza kujikwamua kiuchumi .”amesema .

“Natumia fursa hii kumshukuru kwa dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kiuchumi na kusimamia sera zinazolenga kuwainua wananchi wa kipato cha chini.”amesema Meya Iranghe.

Ameongeza kuwa, uongozi wake umeleta matokeo chanya katika upatikanaji wa fursa za maendeleo, hususan kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha amefafanua kuwa, Jiji la Arusha litaendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inawafikia walengwa kwa ufanisi zaidi na kuleta matokeo chanya katika maisha ya wananchi.