Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wasichana wengi katika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wamejikuta wakilazimika kuachana na ndoto zao za elimu kutokana na mimba za utotoni, jambo linalochochewa na mila potofu zinazoendelea kuenziwa kwa kisingizio cha kulinda utamaduni.

Kijiji cha Kidoka, baadhi ya desturi kama unyago na jando zimegeuka kuwa chanzo kikuu cha changamoto hizo, huku mafundisho ya ngoma hizo yakihusisha maudhui ya mapenzi na ndoa kwa watoto ambao bado hawajakomaa kimwili wala kiakili.

Sheikh Salamu Hando, mkazi wa kijiji hicho, anaeleza kwa uchungu jinsi jamii inavyowaharibu watoto kupitia ngoma hizi.

“Tunawaambia watoto kuwa sasa ni watu wazima, huku tukiwafundisha stadi za ndoa na tendo la ndoa. Hili linawachanganya na kuwafanya waingie mapenzi kabla ya wakati,” amesema Sheikh Hando.

Hali hiyo imebainika katika mdahalo wa wazi ulioandaliwa na mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Agha Khan Foundation kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, ukiwaleta pamoja wazee wa kimila, viongozi wa dini, watu maarufu, wawakilishi wa serikali za vijiji, vikundi vya kijamii na wawakilishi kutoka vituo vya taarifa na maarifa ili kujadili namna ya kuondoa vikwazo vya kijinsia na kulinda haki za mwanamke na watoto.

Arafa Hukomo, mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa kijijini Kidoka, ameeleza kuwa kukosekana kwa sheria kali dhidi ya mila hizo kumeendelea kuwaingiza watoto wa kike katika hatari ya kupata ujauzito mapema na kuacha shule.

“Matokeo yake ni kukatizwa kwa safari yao ya elimu na kuathiri uwezo wao wa kujitegemea baadaye,” amesema.

Vijana wa kiume pia hawajasalimika. Wengi wao hulazimika kuacha shule na kuelekea mijini kutafuta ajira zisizo rasmi, hali inayowatumbukiza katika maisha magumu na kuwaweka mbali na ndoto zao za baadaye.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa kijiji hicho, Samalu Lupande, ameainisha kuwa umasikini wa kaya unachangia pakubwa matatizo haya.

“Wazazi huona elimu ni mzigo, hivyo huwashawishi watoto wasome kwa kiwango cha kawaida tu au waachane kabisa na shule ili wasaidie shughuli za kiuchumi nyumbani,” amesema.

Lupande ameongeza kuwa hali hiyo huwafanya baadhi ya watoto wa kike kukubali msaada kutoka kwa watu wanaowalaghai kwa fedha au mahitaji ya shule kwa masharti ya ngono.

“Hii ni hatari kwa maendeleo ya jamii, kwani inaharibu kizazi kabla hata hakijajengwa,” ameonya.

Kwa upande wake, Vera Assenga kutoka TGNP, amesisitiza kuwa si kila mila ni potofu, bali ni muhimu kuchuja yale mafundisho yanayokinzana na haki na ustawi wa watoto.

“Ngoma za utamaduni zinaweza kubaki kama sanaa, lakini maudhui yake yafanyiwe marekebisho. Tukiweka sheria rafiki kwa mtoto wa kike, tutaweza kulinda maisha yao na bado tukadumisha utamaduni wetu,” amesema.

Deogratius Temba, mwezeshaji wa mradi wa Tuinuke kwa Pamoja, amesema mijadala kama hiyo inalenga kuamsha jamii kijamii na kiakili ili kuchukua hatua za kubadili mwenendo wa mila na desturi zinazodhuru watoto.

Mdahalo huo umeibua mwamko mpya katika wilaya ya Chemba mwamko wa kuhoji, kuchuja, na kubadili mila zenye madhara kwa watoto. Ni wazi sasa kuwa jamii hiyo inahitaji mabadiliko ya haraka, ili kuwapa watoto nafasi ya kutimiza ndoto zao bila vikwazo vya kimila.