Na Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amesema milango ya uwekezaji wa nishati safi ya kupikia ipo wazi kwa wadau wanaotaka kuwekeza.

Amesema hayo ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake na wadau mbalimbali wa masuala ya hifadhi ya mazingira pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba waUmoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaofanyika katika Jiji la Belem, Brazil.

Prof. Msoffe akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Burn Manufacturing Bi. Caroline Amollo ambayo inajihusisha na utengenezaji wa majiko ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania amemshukuru na kupongeza kwa shughuli hizo.

Alimuleza mdau huyo kuwa Serikali ya Tanzania inatambua jitihada za wadau wa maendeleo kama kama hao katika kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu kwa wananchi kote nchini.

“Sote tunapaswa kutambua kuwa nishati safi si tu gesi kama ambavyo watu wengi wanafikiri lakini ni njia yoyote ile ambayo unaweza kuitumia katika kuivisha chakula ili mradi usiharibu mazingira kwa kukata miti ovyo,” alisema.

Kwa upande wake Bi. Caroline alishukuru Serikali kwa kutambua mchango wadau hususan wanaounga mkono juhudi za kukabiliana na changamoto za mazingira kutokana na ukataji wa miti.

Alisema ataendelea kufanya uzalishaji wa majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia na kuwafikia wananchi wengi kwa wakati na kwa gharama nafuu hivyo kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kupikia na wakati huo kuiacha misitu bila kuikata.

Ikumbukwe kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya na mazingira kwa kuhifadhi miti badala ya kuikata kwa ajili ya kuni na mkaa.

Vilevile, lengo la Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2034 kaisi cha asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.

Mkutano huo wa pembezoni umehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi, Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa na wataalamu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.