Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Massauni amesema mpaka sasa jumla ya Miradi 82 ya Biashara ya Kaboni ipo kwenye rejesta na kati ya hiyo, Miradi 4 imeshafika kwenye hatua ya utekelezaji kamili ambapo utasaidia kuiwezesha nchi kupata mapato na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Amesema hayo Dodoma Januari 19, 2025 wakati akiwasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu ya Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira akieleza Biashara ya Kaboni inaendelea kutekelezwa katika Halmashauri mbalimbali zikiwemo Halimashauri za Wilaya za Tanganyika, Kiteto, Karagwe, Uvinza na Mbulu ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo ni Mhe. Jackson Kiswaga.
Biashara ya Kaboni ni mfumo wa kiuchumi unaoruhusu uuzaji na ununuzi wa Viwango vya Kaboni. Lengo lake ni kupunguza gesijoto (Green House Gases) angani. Mradi wa Kaboni maana yake ni mradi wowote unaotekelezwa kwa ajili ya kuzalisha Viwango vya Kaboni (Carbon credits) vinavyotambulika kimataifa.
Miongozi mwa faida zinazotokana na Biashara ya Kaboni ni kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na uhifadhi wa Mazingira, kuimarisha Uchumi, Maisha ya Jamii, Sera, Teknolojia na Ubunifu.
Mhe. Masauni ameongeza kuwa kutokana na biashara hiyo, maendeleo mbalimbali yamepatikana ikiwa ni pamoja na kurudisha uoto wa asili, kujenga majengo ya kutoa huduma za kijamii, na kuchochea upunguzaji wa hewa ukaa.

‘’Kituo kina jukumu la usajili wa Miradi ya Kaboni, Uthibitishaji na Uhakiki wa Viwango vya Kaboni na Gesijoto nyingine kwa kuandaa Miongozo ya Kisayansi inayohusisha kupanga na kuelekeza aina mbalimbali za usimamizi, sera na kujenga uwezo katika masuala ya kiufundi ya Mfumo wa Usajili, Upimaji na Uhakiki (MRV) wa Viwango vya Kaboni na Gesijoto nyingine,” amesema Mhe. Masauni.
Hatua za uanzishwaji wa Mradi wa Kaboni ni pamoja na kuwasilisha maombi ya wazo la Mradi, kuandaa na kuwasilisha andiko la awali la Mradi, Kuandaa na kuwasilisha andiko la Mradi kwa mujibu wa viwango stahiki vya kimataifa, Kuwasilisha andiko la Mradi lililoandaliwa kwa mamlaka ya usimamizi kwa ajili ya kupata idhini pamoja na Kuanza na kutekeleza shughuli za Mradi ndani ya miaka 2 baada ya kupokea barua ya idhini kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Mazingira.
Miradi ya Kaboni inaweza kuanzishwa katika sekta za nishati, uchukuzi, misitu, udhibiti wa taka, viwandani na matumizi ya bidhaa, uchumi wa buluu na kilimo. Mifano ya Miradi ya Biashara ya Kaboni ni pamoja na Uhifadhi wa misitu, Upandaji miti, matumizi ya nishati safi, matumizi ya teknolojia na usafirishaji rafiki.
NCMC kina majukumu mengi ikiwemo kuratibu masuala yanayohusiana na Biashara ya Kaboni na usimamizi wa Gesijoto kwa kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa uzalishaji wa Gesijoto na Biashara ya Kaboni nchini.



