🔸Zaidi ya Shilingi Bilioni 33.81 zatekeleza miradi ya maendeleo ya jamii
MKOA wa Mara umeendelea kunufaika na uwekezaji wa Sekta ya Madini baada ya kutekeleza zaidi ya miradi 398 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 33.81 katika wilaya zote ndani ya kipindi cha miaka minne chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatua inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi.
Akizungumza hivi karibuni kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Afisa Mazingira, Byalugaba Chakupewa alisema utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka migodi ya kati na midogo umeendelea kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali.

Alisema michango ya kampuni za uchimbaji madini imeendelea kusaidia miradi ya kijamii, ikiwemo Shilingi milioni 40 zinazotolewa na ZEM (T) Co Ltd katika Wilaya ya Butiama, Shilingi milioni 40 za Polygold kwa Halmashauri ya Musoma, na Shilingi milioni 125 zinazotolewa na MMG Gold Mine kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Seka, madarasa Kalusenyi, ofisi ya kijiji cha Kaboni pamoja na jiko la gesi katika Shule ya Sekondari Kasoma.
Aidha, alisema kupitia mpango wa vijana wa Mining for the Brighter Tomorrow (MBT), vikundi 53 vyenye jumla ya vijana 1,998 vimepatiwa leseni za uchimbaji mdogo, hatua inayoongeza ajira na ushiriki wa vijana katika uchumi wa madini.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, alisema mgodi huo umetumia Shilingi bilioni 26 kutekeleza miradi ya jamii kuanzia mwaka 2019 hadi 2025.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo imetenga Dola milioni 1.8 kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wanaoishi jirani na mgodi, sambamba na kulipa zaidi ya Shilingi bilioni 2 za mrabaha kila robo mwaka.

Alisema zaidi ya watoto 500 tayari wamenufaika na mfuko wa elimu wa mgodi huo, ingawa bado kuna changamoto ya baadhi ya jamii kushindwa kutambua vipaumbele vya maendeleo, hali iliyosababisha Barrick kuanzisha mpango mkakati wa miaka mitano unaolenga kushughulikia mahitaji ya msingi kama upatikanaji wa maji na barabara.
Uhadi alibainisha kuwa mgodi umejenga tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita 300,000 linalohudumia vijiji vya Matongo, Mjini Kati, Nyabichune na Nyang’oto, huku kiwango cha manunuzi ya wazawa kikifikia asilimia 91, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ‘local content’ katika shughuli za mgodi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Nyamongo, Dotto Manyeli, alisema mradi huo wa maji umeajiri watu 20 na umewezesha taasisi za elimu na afya kupata huduma ya maji ya uhakika na ya gharama nafuu.
Kwa upande wa wazawa wanaotoa huduma, Mkurugenzi wa Roebray Enterprises & Supplies Ltd, Rhobi Alphonce, alisema licha ya mafanikio makubwa waliyopata katika kuhudumia mgodi, wamekumbana na changamoto za usimamizi wa wafanyakazi, hali iliyowalazimu kuboresha mifumo ya ajira ili kulinda usalama na siri za kampuni.
Katika sekta ya elimu, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyabichune, Innocent Mushi, alisema maabara iliyojengwa na Barrick North Mara imeleta mabadiliko makubwa katika ufundishaji wa masomo ya sayansi, ambapo wanafunzi sasa wanafanya mazoezi kwa vitendo tofauti na ilivyokuwa awali.
Alisema hatua hiyo imeongeza ufaulu na kuongeza uelewa wa wanafunzi katika masomo ya sayansi.





