Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 jumla ya miradi kumi ya kuhifadhji mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 97.6 imetekelezwa na kukamilika Zanzibar.
Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma leo Februari 04, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Rashid Habib Ali aliyetaka kufahamu Zanzibar inanufaikaje na fedha za mazingira zinazotolewa na wafadhili.
Mhe. Dkt. Dugange ameliarifu Bunge kuwa utekelezaji wa miradi ya mazingira umeleta manufaa kwa jamii kwa kuongeza kipato kupitia shughuli mbadala hivyo kuongeza uwezo wa jamii katika uhifadhi wa mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi
Akiendelea kujibu swali la mbunge huyo alifafanua kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umechangia katika ukuaji wa uchumi kwa maendeleo endelevu na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Dugange alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipokea fedha kutoka kwenye Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi na wafadhili mbalimbali wakiwemo Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF), Mfuko wa Mabadiliko ya tabianchi (GCF), Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Aidha, alibainisha kuwa fedha zinazopatikana zimekuwa zikitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Hivyo, alisema Serikali imeendelea kuandaa miradi kwa ajili ya kutafuta fedha kupitia vyanzo mbalimbali ambapo hadi sasa jumla ya miradi mitatu yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 62.6 ipo kwenye hatua za awali za maandalizi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alisema fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mazingira zinagawanywa kwa kuzingatia uwiano wa uhjtaji wa pande zote mbili za Muungano.
Alisema mkakati wa Serikali ni kuboresha maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi hususan ya kwenye fukwe za bahari ambako maji huingia kwenye makazi ya wananchi na kuleta madhara.
Mhe. Dkt. Dugange alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Ali aliyeuliza ni upi mgawanyo wa utekelezaji wa miradi Tanzania Bara na Zanzibar.



