Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD, limesema misaada ya maendeleo ilipungua kwa kiwango cha kihistoria kwa asilimia 23.1 mwaka uliopita.
Shirika la OECD lenye makao yake makuu mjini Paris nchini Ufaransa lilisema data zake za awali zilionyesha misaada rasmi ya maendeleo na nchi wanachama wa kamati yake ya msaada wa maendeleo ilifikia dola bilioni 174.3 mwaka jana, ikiwa imeshuka kwa mwaka wa pili mfululizo.
Shirika lisilo la kiserikali la kupambana na umaskini, Oxfam, limekosoa kupunguzwa huko, likitaja jukumu muhimu la misaada hiyo katika kupambana na magonjwa kama vile virusi vya ukimwi na malaria.
Kiongozi wa fedha za maendeleo wa Oxfam, Didier Jacobs, amesema taasisi ya afya duniani ya Barcelona ilikadiria kwamba kupunguzwa kwa misaada duniani kwa kiwango hicho kutawaua mamia ya maelfu ya watu.
Amezitaka serikali kurejesha bajeti zao za misaada na kuimarisha mfumo wa utoaji wa misaada ya kibinadamu wa kimataifa unaokabiliwa na mgogoro wake mkubwa zaidi katika miongo kadhaa.


