Na Pendo Nguka,JamhuriMedia Dar es Salaam

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini (DCP), David Misime ameeleza uhitaji wa mchango mkubwa wa waandishi wa habari hasa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kuzingatia sheria na kanuni.

Misime amesema hayo leo Agosti 21, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji.

Misime ameeleza kuwa waandishi wa habari wana jukumu la kuzingatia weledi, maadili, na miiko ya taaluma yao katika kutoa taarifa kwa umma.


“Taarifa hizo zinazotolewa zinapaswa kuwa za kweli, zenye kuelimisha na kufafanua sheria, miongozo na kanuni zinazolenga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na usalama,” alisema DCP Misime.

Aidha DCP Misime amebainisha kuwa Jeshi la Polisi lina jukumu kubwa kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi, kuhifadhi ushahidi, na kufanya ukamataji wa wahalifu watakaovuruga mchakato wa uchaguzi,

Kufuata mikataba mbalimbali ya kikanda inayolenga kulinda amani, kudhibiti na kutanzua uhalifu kutoa ulinzi kwenye mikutano ya kampeni, kutoa usalama kwa wagombea na wapiga kura wakati wa zoezi la upigaji kura.

Pia kushirikiana na jamii katika kubaini, kuzuia, na kutatua vyanzo vya vurugu, kutoa taarifa kwa umma kwa masuala yanayohitaji ufafanuzi, kushiriki kwenye midahalo mbalimbali ya kujenga uelewa wa masuala ya kiusalama, kutoa mafunzo kwa askari ili wawe tayari kutoa huduma bora kwa raia wote bila upendeleo, wakiwemo waandishi wa habari, kuhakikisha askari wanazingatia uzalendo na utaifa wanapotekeleza majukumu yao.

DCP Misime pia amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa uadilifu na uzalendo katika kulinda taifa, na kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu, na usalama.

“Kila mtu ana umuhimu wa kuheshimu taaluma ya kila mmoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi”amesema.

Aidha, amewakumbusha waandishi kuepuka kutoa taarifa za kufikirika zisizo na msingi.

“Waandishi wanatakiwa kujielimisha kwa kusoma Sheria ya Makosa ya Mtandaoni pamoja na Sheria ya Usalama wa Taifa ili wawe na uelewa sahihi wa mipaka ya kazi zao katika mazingira ya uchaguzi,”amesema Misime.