*Wasira asema madiwani, wabunge wasubiri mchujo kura za maoni

*Asisitiza haki kutendeka katika kupata wagombea , akemea rushwa

*Atoa rai kwa wananchi kuwapuuza viongozi wa kisiasa wanaohubiri chuki

*Awapiga kijembe CHADEMA, awaambia mchawi wao ni wao wenyewe

Na Mwandishi Wetu, Nyasa

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu mkakati wa ‘Mitano Tena’ ni kwa mgombea urais, Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, lakini wabunge na madiwani wasubiri mchujo ndani ya Chama.

Wasira aliyaeleza hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani kilichohusisha viongozi wa CCM Wilaya ya Nyasa, katika mji wa Mbamba Bay mkoani Ruvuma jana, ambako anaendelea na ziara ya kuimarisha Chama.

“Niwaambie wana CCM wenzangu tunaposema mitano tena ni kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya urais na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi lakini kwa wabunge na madiwani wasubiri mchujo ndani ya Chama na mwaka huu tumeongeza idadi ya wapiga kura. Kwa mfano hapa Nyasa walikuwa wapigakura za maoni 900 lakini sasa wako 1,3000.”

Wasira alisema kupata wagombea safi ndani ya Chama wa udiwani na ubunge ni vema wakachaguliwa kwa utaratibu wa haki huku akisisitiza ‘mitano tena’ sio kwa watu wote ”Sio kila mtu ni mitano tena bali mitano tena ni kwa Rais Samia, wengine tunachujana.”

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Stephen Wasira akizungumza na Wanachama pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM Wilaya ya Tunduru, Leo Juni 10, 2025 akiwa Katika Tiara make ya kukagua Uhai wa Chama Mkoa wa Songea

Akifafanua zaidi, Wasira alisema mabalozi wa CCM wana kazi ya kuchagua wagombea safi kupitia kura za maoni ambao watauzika mbele ya wananchi na sio wagombea ambao wanatokana na kununua kura.

“Heshima ya wajumbe ni anayesikiliza watu walionyuma yake, ni kupiga kura kwa mtu ambaye wananchi wanamtaka na katika majina matatu ambayo yatapendekezwa kupitia kura za maoni atapatikana mmoja ambaye atakuwa diwani au mbunge kwa miaka mitano.

“Kuna diwani amesema hapa kuwa wamefanya kazi nzuri na wanaomba ruhusa waendelee. Hakuna mtu anakataa ruksa lakini ruhusa haitolewi na mimi bali inatolewa na wananchi waliokupigia kura. Mimi nikimaliza (ziara) naondoka lakini wapigakura wanabaki na ndio watasema diwani amefanya kazi nzuri tunataka arudi na wale wapigakura wa kata yako watasema hivyo ndivyo.”

Aliongeza kuwa Chama kinataka viongozi ambao watasimama katika nafasi za uwakilishi kwa sababu wametumwa na wananchi na kwamba wakienda kwa ridhaa ya wananchi hawawezi kupotea kwa sababu watajua nyuma yao kuna watu ambao wanawatazama.

Makamu Mwenyekiti Wasira alisisitiza kwamba Chama kinataka kwenda katika uchaguzi mkuu na kushinda kwa kishindo bila bila ya gharama nyingi wala migogoro.

“Itakapofika Oktoba kwenye urais tunatiki kwa Dk. Samia na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi na kwa wabunge mnatiki kwa wale mtakaowapigia kura, kwa udiwani tunatiki kwa wale watakaokuwa wameshinda katika mshike mshike wa kura (kura za maoni) kwenye kata.

Pamoja na hayo, alisisitiza vikao vya Chama kata, wilaya na mkoa vitende haki kwa wanachama. ”Watendeeni haki wale wanaostahili haki msiwalete wale ambao wanafikiria rushwa ndio jibu maana vitabu vyote vya imani za dini Waislam na Wakristo wanapinga rushwa.“

HATUBAGUANI

Wasira alieleza kuwa Tanzania ni nchi ambayo watu wake wananshi bila ya kubaguana kwa dini, rangi au kabila na kwamba hayo ni matunda yaliyotokana na kazi nzuri ya kujenga umoja na mshikamano iliyofanywa na waasisi wa taifa.

Aliwataka wananchi kuwaepuka viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakihubiri kuvuruga amani, umoja na mshikamano uliojengwa na kudumu nchini tangu kuasisiwa kwake.

“Tuna makabila 126 lakini tunazungumza lugha moja, sasa ukikuta mtu ana akili timamu tena ni kiongozi wa kisiasa anataka kubomoa umoja huu huyo mwambieni amekosea njia, mwambie umepiga ‘wrong namba.

“Unajua unapiga halafu unaambiwa namba uliyopiga haipatikani. Sasa mwambie hapa ulipopiga namba ambayo haipatikani. Niwaambie mafanikio yetu kama Chama katika Afrika ni kuwaleta watu pamoja na wakaishi kama familia moja na msingi wa umoja wetu ndio siri ya amani yetu,” alieleza.

Akiizungumzia CHADEMA baada ya Rais Samia kuingia madarakani, Wasira alisema baada ya Rais Samia kuingia madarakani aliamua kuja na mfumo wa maridhiano na Chadema wakawa na maombi mbalimbali ikiwemo kutaka kuachiwa kwa viongozi wao waliokuwa wamekimbia nje ya nchi warudi nchini na wawe salama.

“Walio nje warudi bila masharti na wamerudi wote wako nchini na wako salama kulingana na tabia zao maana kwamba warudi wakae salama sio kwamba wana uhuru wa kuvunja sheria, hapana ukivunja sheria maridhiano yanawekwa kando na sheria inachukua mkondo wake.

Akizungumza kinachoendelea CHADEMA, Wasira alisema tangu walipomaliza uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wao wamekuwa na misuguano.

“Baada ya ule uchaguzi wao kila mtu amechukua chake na mtu anaitwa Lissu naye akachukua virago vyake na sasa hawako pamoja ndio wakasababisha kupatikana CHAUMA…

“Afrika hakuna anayekufa bila mchawi, mchawi wa Chadema ni Chadema wenyewe kwa kuwa hawasikilizani na wanachama wao wanawaambia tukagombee ubunge wanasema mna uchu wa madaraka tena wanaosema hivyo ni vijana wadogo.

“Godbless Lema amekuwa kwa mbunge miaka 10, Tundu Lissu amekuwa mbunge 10, John Heche miaka mitano. Hivyo wamekuwepo bungeni, Mnyika amekaa bungeni miaka 10. Vijana wenzao wanataka kujaribu kugombea wanasema wana uchu wa madaraka, wale watu wabinafsi,” alisema.

Alisisitiza kuwa, hao ndio wamefanya chama hicho kisambaratike, hivyo aliwashauri watafute mganga wa kuwaagua.