Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MIKATABA ya maandishi ya ajira kwa wafanyakazi wa nyumbani imetajwa kuwa ni kilio cha wengi kisichokuwa na matumaini kwao kutokana na waajiri wengi kuruka vigingi vya kuingia katika makubaliano nao huku Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, ikieleza kuwa mfanyakazi yeyote anayefanya kazi kwa zaidi ya saa 45 kwa wiki anapaswa kuwa na mkataba wa ajira na kulipwa posho ya masaa ya ziada.

Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa ellimu rika wa wafanyakazi wa nyumbani wapatao 25 kutoka mikoa sita kuwasilisha kilio hicho katika warsha ya mafunzo ya wafanyakazi hao yaliyoratibiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ,Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) kwa kushirikiana na Serikali pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhi, Hotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU).

Wamesema asilimia kubwa ya wafanyakazi hao wanamikataba ya midomo na sio ile ya maandishi kama sheria inavyowataka waajiri kufanya hivyo kusababisha kukosa haki zao za msingi.

Desdelia Simon Mfanyakazi wa nyumbani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Nyumbani Mkoani wa Morogoro amesema ukosefu wa mkataba wa maandishi ni moja ya Changamoto kubwa ambayo wanakumbana nayo huku mkataba huo unakuwa umebeba haki zao.

Amesema endapo waajiri wanapokuwa hawaingii mikataba na wao wanajikuta wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutolipwa mshahara kwa wakati na waajiri wengine kuwanyima kabisa, unyanyasaji wa kijinsia, kukosa likizo kama wafanyakazi wengine waajiri wakidai kuwa hakutakuwa na mtu mwingine wa kufanya kazi wanazofanya kwa kipindi cha likizo pamoja na kuwaita majina machafu.

Simon amesema kuna haja ya waajiri wakaona kuna umuhimu wa wao kuingia mkataba wa maandishi na wao ili kuwasaidia wafanyakazi wa nyumbani nao kupatiwa haki zao kama zilivyokwa waajiri wa sekta nyingine.

”Utakuta Mfanyakazi wa nyumbani anahitaji kwenda likizo anashindwa kwenda kutokana na kutokuwa na mkataba na endapo atafanya hivyo kibarua chake kinaweza kuishia hapo kutokana na mwajiri kutoamini kama hatorudi kazini na kushindwa kumshtaki.y

”Tunafanya kazi za makubaliano ya mdomo tu ambayo hayana uhalali wa kimaandishi hali inayopelekea kukosa haki zetu za msingi kwani kazi tunazofanya ni sawa na kazi nyingine,”amesema.

Amesema waajiri wengi wamekuwa wakikimbia kuingia katika mikataba ya maandishi kutokana na kuona mikataba hiyo itaweza kuwafunga wao na kuwatetea wafanyakazi wa nyumbani jambo ambalo si kweli.

”Waajili wengi wanafikilia kuwa endapo wanapoingia mkataba na sisi kwamba wao ndio wanaminywa na mikataba hiyo,jambo ambalo sio kweli bali mikataba hiyo inakuwa inafaida kwa pande zote mbili kati ya waajiri na wafanyakazi wa nyumbani,”amesema

Jenifer Mtanga Mfanyakazi wa Nyumbani kutoka Mkoani Dodoma amesema kwa upande wake ndani ya mwaka mmoja ameweza kupata mwajiri ambaye tayari ameingia nae mkataba wa maandishi katika kufanya kazi nae.

Anasema mkataba wa maandishi umekuwa na msaada mkubwa kwake kutokana kuwa na likizo,Mshahara wake kulipwa kwa wakati pamoja na kupatiwa muda wa mapumziko kama wafanyakazi wengine wa sekta nyingine wanavyopatiwa.

”Awali nilifanya kazi na waajiri tofauti tofauti na wa mwisho alikuwa Mwanamke nilijikuta nafukuzwa kazi bila kujua kosa langu lolote huku mshahara wangu niliambiwa kuwa nitatumiwa na kazi kusimamishwa.

”Niliumia sana lakini sikuwa na namna ilinibidi kuja kufatilia kwanini aliamua kunifukuza kazi mwajili wangu ndipo niligundua kuwa muajiri wangu alikuwa na wasiwasi na mimi kuwa naweza kumchukua mume wake jambo ambalo lilinisikitisha sana”amesema

Mtanga amesema aliamua kukaa nyumbani ambapo mwaka jana mwishoni ndipo alipobahatika kupata mwajiri mpya ambaye alikuwa akifatilia masuala ya Mafunzo ya CHODUWA na kumpatia mkataba wa maandishi na kulipwa kiasi cha Sh. 150000.

Amesema hadi sasa ni mwaka mmoja amekuwa anafanya kazi kwa mwajiri huyo ambapo anapatiwa haki zake za mfanyakazi wa nyumbani kama wanavyopata wafanyakazi wengine ikiwemo Likizo,Ruhusa za kutoka na kuhudhuria mafunzo ya CHODUWA pamoja na haki zake za msingi huku mshahara wake ukibaki palepale.

Kwa Upande wake Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka CHODAWU Taifa,Asteria Gerald amesema mkataba ni nguzo kubwa ya majadiliano baina ya mwajiri na mfanyakazi wa nyumbani katika kulinda haki ya kila mmoja.

Amesema katika ajira yoyote migongano uwa haikosekani hivyo endapo mkataba unapokuwepo unasaidia kwa kiasi kikubwa kujua ni kiasi gani mfanyakazi wa nyumbani analipwa na hata akiripoti katika ofisi za maamuzi mwajiri anajua namna ya kujitetea.

”Mkataba inakuwa ni rahisi katika kutatua migogoro,mnaweza kukubaliano kwa mdomo unamlipa mfanyakazi wa nyumbani kiasi cha Sh. 50000 lakini baadae anaweza kuja kukuruka kuwa mlikubaliana 100,000 na ikifika ngazi ya maamuzi ni lazima mwajiri utalipa kiasi hicho kwa sababu haukuwa na mkataba wa maandishi.

”Mkataba wa maandishi unampa wajibu mfanyakazi anapopaswa kuondoka kwa mwajiri kutoa taarifa kabla ya mwezi mmoja na endapo ataondoka bila kutoa taarifa anapaswa kumlipa mwajiri wake,hivyo mkataba wa maandishi unalinda pande zote mbili Mfanyakazi wa Nyumbani pamoja na Mwajiri wake,”amesema

Naye Muamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Herman Komba amesema sheria ya kazi,ajira na mahusiano mahali pa kazi imeeleza namna ambavyo mahusiano ya kiajira inavyotakiwa kuanza kwa muajiri kutoa Mkataba wa ajira kwa mfanyakazi.

Amesema ndani ya Mkataba huo wa ajira sheria imeeleza vitu vinayopaswa kuwepo ni pamoja na majina ya muajili na muajiriwa,Anuani ya Makazi,Kiwango cha Mshahara ,Muda wa kufanya kazi na Likizo.

”Lakini imekuwa ni changamoto kwa waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani kutokuwapa mikataba wafanyakazi wao,bali wengi wao uwapatia mikataba ya makubalianao yaani ya mdomo ambapo kisheria nayo inakubalika kulingana na mazingira.

” Ila Sheria iliweka wajibu kwa mwajiri kutoa mkataba endapo atakiuka takwa hilo kile atakachosema mfanyakazi ndicho kitakuwa kimepewa kipaumbele mfano akisema makubaliano yao yalikuwa kulipwa 80000 badala ya 50000 sheria itatoa maamuzi kulingana na mwajiriwa atakachosema,”amesema.