Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, akiambatana na baadhi ya Wakuu wa Divisheni na Vitengo kutoka Halmashauri, ameendelea na zoezi la kufanya mikutano ya ana kwa ana na wajasiriamali wadogo wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara katika Kata ya Mkuza na Kongowe.

Lengo la ziara hiyo ni kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wajasiriamali hao ili kuwawezesha kukuza biashara zao kwa uendelevu na tija.

Akiwa katika Kata hizo, Dkt. Shemwelekwa alizungumza moja kwa moja na wafanyabiashara wadogo na kubaini changamoto kubwa wanayokumbana nayo – hasa ile ya upatikanaji wa mitaji ya kuaminika. Wafanyabiashara hao walieleza kuwa hulazimika kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za kifedha zenye riba kubwa maarufu kama “kausha damu”, jambo ambalo limekuwa likiwakwamisha.

Wamemuomba Mkurugenzi awasaidie kupata mitaji yenye masharti nafuu na isiyowadidimiza kiuchumi.

Akijibu kilio hicho, Dkt. Rogers Shemwelekwa amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ina zaidi ya shilingi Bilioni Moja zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupitia mikopo isiyo na riba.

“Nawahamasisha mujiunge kwenye vikundi vya watu watano ili muweze kufaidika na fursa hii ya mikopo isiyo na riba. Pesa ipo na nia yetu ni kuona biashara zenu zinakua,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Aidha, ameeleza kuwa kuanzia kesho, Maafisa Maendeleo ya Jamii wataanza kazi ya kuwaandaa wajasiriamali hao kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote zinazohitajika, ili waweze kupokea fedha hizo ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo.

Wafanyabiashara hao wamempongeza Mkurugenzi kwa hatua hiyo ya haraka na ya kivitendo, wakieleza kuwa ni mkombozi wa kweli kwao. Wameomba aendelee na moyo huo wa kuiletea maendeleo Manispaa ya Kibaha.