Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaendelea jijini New York ambapo viongozi mbalimbali wa dunia wanahudhuria na wanatarajiwa kuhutubia katika kikao hicho cha 80 kinachogubikwa na vita vya Gaza na Ukraine.

Kikao hicho Baraza Kuu la Umoja la Mataifa killianza siku ya Jumatano (Septemba 10) kwa ufungaji wa kikao cha 79 na kuapishwa rasmi kwa rais mpya wa Baraza hilo, Annalena Bearbock, aliyechukuwa wadhifa huo wa mzunguko kutoka kwa Philemon Yang.

Yang, waziri mkuu wa zamani wa Kameruni na ambaye alishikilia nafasi hiyo kwa jina la uwakilishi wa Afrika, aliiambia hadhara hiyo kuwa mkataba ulioianzisha taasisi hiyo na Umoja wa Mataifa wenyewe ni alama ya ahadi ya pamoja kwamba “dunia inaweza kuwa bora zaidi, ikiwa viongozi watatimiza wajibu wao kuitekeleza ahadi hiyo.”

Maudhui ya kikao hiki cha 80 cha Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo linaadhimisha pia miaka 80 tangu kuundwa kwa taasisi hiyo ni “Tukiwa wamoja, tunakuwa bora zaidi: Miaka 80 na zaidi kwa ajili ya amani, maendeleo na haki za binaadamu.”

Akipokea kijiti cha uongozi wa Baraza hilo, Baerbock , aliuita mwaka huu kuwa wa “utekelezaji, mageuzi na ujenzi wa Umoja wa Mataifa unaohitajika kwa miaka mingine 80 ijayo.”