Rais wa Urusi na Ukraine wanatazamiwa mnamo siku chache zinazokuja kufanya mazungumzo ya amani ambayo yatakuwa ya kwanza tangu Moscow ilipoivamia Ukraine zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Matumaini ya mkutano huo kati ya Rais Vladimir Putin wa Urusi na Volodymyr Zelensky wa Ukraine yamefuatia mazungumzo marefu yaliyofanyika jana mjini Washington yakiwaleta pamoja Rais Donald Trump wa Marekani na viongozi kadhaa wa mataifa ya Ulaya.

Baada ya mkutano huo kwenye Ikulu ya White House, Trump alisema alimpigia simu Rais Putin na kukubaliana naye juu ya umuhimu wa kuitishwa mkutano wa ngazi ya juu kati ya Urusi na Ukraine.

Rais Zelenskyy wa Ukraine amesema yuko tayari kukutana na Putin na amemshukuru Trump na viongozi washirika wa Ulaya kwa kuongoza jitihada za kumaliza vita nchini mwake.