Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa nchi za Falme za Kiarabu, Luteni Jenerali Eisa Saif Mohamed Bin Ablan Almazrouei amefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania leo tarehe 14 Julai 2025.
Jenerali Almazrouei alipokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda.
Mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga Jijini Dar es Salaam, Luteni Jenerali Almazrouei alipokea salamu ya heshima na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake.
Wakati wa mazungumzo yake mafupi na ujumbe huo toka Falme za Kiarabu ofisini kwake Upanga, Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda alieleza umuhimu wa ushirikiano wa Kijeshi uliopo baina ya Mataifa haya mawili kuwa unaendelea kudumishwa.
Jenerali Mkunda amesema JWTZ linajivunia, ushirikiano uliopo katika kukabiliana na matishio ya kiusalama kama vile ugaidi na usafirishaji haramu wa binadamu katika nchi mbili hizi. Aidha, maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na Mafunzo, Utafiti, Utamaduni na Michezo, na kuimarisha ulinzi wa mipaka.
Aidha, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa UAE Luteni Jenerali Almazrouei ameshukuru ukarimu alioneshwa na mwenyeji wake Jenerali Jacob Mkunda na kusisitiza kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Majeshi haya mawili.
Luteni Jenerali Almazrouei yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya kudumisha ushirikiano uliopo baina ya majeshi haya mawili.




