Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Songwe Jabir Makame, amewataka wananchi wa mkoa huo na kamati ya Ulinzi na Usalama kuwa macho na kutocheka na yeyote anayehujumu miradi ya Umwagiliaji.
Amesema fedha zinazowekezwa na Serikali katika miradi hiyo ni nyingi na Imelenga kupunguza umaskini kwa wakulima hivyo anayehujumu miradi ya Umwagiliaji anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa analihujumu Taifa
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Jabir amesema hayo wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi wa mradi wa skimu ya umwagiliaji Naming’ongo uliopo kata ya Chitete mkoani humo.

Amesema mradi huwo wa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 24 utatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambapo ndani ya mradi huo kutakuwa na ujenzi wa barabara za ndani, ajira zaidi ya 2000 huku wakulima zaidi ya 6000 wakiwa wanufaika wa eneo hilo.
“Wananachi na kamati ya ulinzi na usalama tuchukue hatua kwa watu wanaoharibu miundombinu ya Umwagiliaji, kamati yetu ichukue hatua ili kukomesha tabia hizo, shughuli za ufugaji zisizo rafiki na kuleta madhara katika vyanzo vya maji na kuharibu miundombinu zikomeshwe”, amesema.
Amewataka halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha kunakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi , ili mradi utakapokamilika uvutie uwekezaji katika maeneo ambayo yamepimwa na kuepusha uharibifu wa mazingira maeneo ya miradi yote ya Umwagiliaji.

Jabir amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi inaanza mara moja na vifaa vilivyopo eneo la mradi vifanye kazi kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa na kufanya kazi kizalendo, ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa muda wa miezi 24, kuanzia Septemba mwaka 2025 hadi Septemba 2029.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Momba Elias Mwandobo amesema, hatua ya mradi huo na miradi yote ya Umwagiliaji ni miradi ya kimkakati iliyolenga kugusa mwananchi mmoja mmoja na kubadilisha uchumi wa wilaya, mkoa na Taifa katika kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwa na kilimo biashara.
“Tulikuwa na kilimo cha kupiga ramli kwa kutokuwa na uhakika wa mvua, miradi hii ya Umwagiliaji inatuletea kilimo cha uhakika hivyo Serikali imekusudia kuongeza tija ya uchumi kupitia kilimo.

“Wananchi wa Kasinde, Naming’ongo, Kamsamba na Msangano pia kuna miradi mikubwa ya Umwagiliaji, zaidi ya bilioni 50 zinawekezwa Wilayani hapa, haina kwa bahati mbaya imelenga kutumia Kilimo kuchochea uchumi na kuongeza uzalishaji, wananchi muwe tayari,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume Raymond Mndolwa amesema utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji inalenga kujibu nia njema ya uwekezaji uliofanywa na serikali ili kuiwezesha Tanzania kulisha Dunia.
Amesema kati ya maeneo ambayo Tume inajenga miradi, ni pamoja na mabonde 22 ambapo Momba ni moja wapo na kuanzia sasa hadi Oktoba kutakuwa na kasi ya kukabidhi miradi kwa wakandarasi ili kufikia adhima ya Serikali katika sekta ya kilimo nchini.
“Mwaka 2023 Tume kulikuwa na ujenzi wa miradi 13 leo hii kuna miradi zaidi ya 700 inayotekelezwa,pia kulikuwa na ujenzi wa miradi mitano pekee wakati wa bajeti ya mwaka 2022/23 leo hii kuna miradi 126 yenye wakandarasi. Bajeti pekee imefikia Trilioni 1.2 na fedha ambazo Tume imepokea ni zaidi ya bilioni 492 na ndani yake kuna VAT, miradi 30 imekamilika huku zaidi ya 60 imefika zaidi ya asilimia 50 na fedha ni bilioni 492, ni wazi matumizi ya fedha za Serikali yako vizuri na yanasimamiwa,”amesema.

Mndolwa amesema katika ujenzi huo kutakuwa na ghala la kuhifadhi nafaka na mashine za kuchakata mazao hayo.
Pia amemtaka Mkandarasi kutoa ajira kwa wazawa na wananchi hao wawe waaminifu ili kuwa na mradi bora huku akisisitiza haja ya wananchi kulinda ardhi zao kwa kutokuuza maeneo na ameahidi kuwa Tume itashirikiana na Wilaya kupima, kutoa hati za mashamba na kuzimilikisha kwa wananchi.
Naye Mhandisi wa NIRC Mkoa wa Songwe John Chacha amesema mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi MBUYA’S CONTRACTORS COMPANY LTD, hatua utaongeza eneo la Umwagiliaji kutoka hekta 1500 hadi kufikia hekta 5000.
“Wakulima 6000 watanufaika moja kwa moja kwa kufanya shughuli za kilimo ndani ya skimu na watu zaidi ya 5000 ambao siwanufaika wa moja kwa moja, ikiwemo wafanyabiashara , watoa huduma ya zana za kilimo hivyo kuongeza tija katika uzalishaji wa mpunga kutoka tani 2.4 kwa hekta ya sasa hadi tani 25 kwa hekta.

Amesisitiza kuwa hatua ya NIRC kujenga ghala na mashine za kuchakata mazao kumelenga kuongeza ukuaji wa viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mpunga, ili kuinua maisha ya wananchi ambao ni wakulima wa Chitete.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Skimu hiyo, Kredo Siwiti ameishukuru Serikali kupitia Tume na Wizara ya Kilimo kwa kuwekeza fedha zaidi ya shilingi bilioni 24, ambazo wananchi wa Kata ya Chitete watanufaika na kuwa na Kilimo Chenge tija.





