-Asisitiza nidhamu, weledi, uzalendo
-Awataka wananchi kuwa raia wema.
Na Byarugaba Innocent, Nyasa DC
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri leo Agosti 22, 2025 amefunga Mafunzo ya Jeshi la akiba yaliyoanza rasmi Aprili 9,2025 yakiwa na Wanafunzi 16.
Mkufunzi Mkuu wa Mafunzo WOII Makame SA amesema kuwa wanafunzi wamejifunza silaha ndogondogo za kivita kama vile Semi Automatic Riffle (SAR), Sub Machine Gun (SMG),Light Machine Gun (LMG),Utimamu wa mwili,Mbinu za Kivita, Ujanja wa porini,Kuzuia na kupambana na rushwa, Usalama wa raia na mali zao, uhamiaji, Zimamoto na uokoaji, Sheria za Jeshi la Akiba, usomaji wa ramani na uchimbaji wa mahandaki.

Akitoa taarifa fupi ya Mafunzo, Kaimu Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Nyasa Meja Isaack Charles Mugomba amesema mafunzo yalianza Aprili 9,2025 yakiwa na wanafunzi 16 baada ya hamasa kufanyika idadi iliongezeka na kufikia 57 kati yake Wanaume 44 na wanawake 13 hata hivyo wanafunzi 2 wanaume waliacha bila sababu.
Akiongea na wahitimu pamoja na halaiki iliyokusanyika kwenye sherehe hizo Magiri amewapongeza wakufunzi kwa kazi nzuri ya kuwanoa wanafunzi kwani wameiva kimafunzo, ukakamavu na weledi wa kijeshi na kuwataka kulitumikia Taifa kwa nidhamu na uzalendo.
“..Ninyi ni askari mmefundishwa Taratibu na sheria za kiaskari kamwe msitumie Mafunzo haya vibaya kwa kuumiza wananchi. Kufanya hivyo mtakuwa mmekiuka maadili ya kiaskari” amesema.

Aidha,Mhe. Magiri amewataka askari kuwa mfano katika Jamii na kuwa mstari wa mbele kwenye shughuli za kijamii,waadilifu na wazalendo namba moja kwa kuwasemea vizuri viongozi ili Kujenga nchi yenye kuheshimika nje na ndani ya Mipaka.
Akijibu risala ya wahitimu, Mhe.Magiri amesema askari wa Jeshi la akiba watashiriki kwenye shughuli mbalimbali za serikali zinazohitaji ulinzi kama kulinda mitihani ya Kitaifa, Uchaguzi, Ziara za viongozi, Mwenge wa uhuru kwa kushirikiana na Jeshi la polisi kuhakikisha usalama unakuwepo mara zote huku akiahidi kuwapa vipaumbele vya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ama Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) watakaokuwa na sifa hitajika
Mhe.Magiri ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 29 Oktoba,2025 na kuwataka kutumia haki yao ya Msingi kikatiba kwa kuwachagua viongozi watakaoleta Maendeleo nchini.

Sambamba na hilo, amewataka wananchi kuchukua tahadhari za kiusalama hasa Taifa linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu kwani Ulinzi wa Taifa letu unategemea watu wote na si askari pekee.
Gwaride la askari wa Jeshi la akiba liliongozwa na MGM Gloria Yohana Mapunda likiwa na gadi mbili. Gadi namba moja iliongozwa na MG Walece James Ndunguru huku gadi namba mbili ikiongozwa na MGM Eofracia Adam Ndomba. Kongole kwa MGM Riziki Said Hassan alikuwa mtunza nidhamu kwa kipindi chote cha Mafunzo.
Aidha, sherehe hizo, zilinogeshwa na onesho kabambe la Kwata ya miguu, Kwata Mchanganyiko na kombati karate iliyodhihirisha ukomavu na utimamu wao kiakili na kimwili na kwamba wapo tayari kwa dharula katika kulinda na kulitete a Taifa.
Sherehe hiyo imehudhuriwa na Kamati ya Usalama Wilaya, Viongozi wa Vyama vya siasa,Wazazi na walezi wa wahitimu, pamoja na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyasa.
