Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
Watu wawili wamefariki dunia na mwingine kujeruhiwa vibaya, huku nyumba kadhaa zikiharibiwa, kufuatia mlipuko mkubwa uliotokea katika banda la kuchomelea vyuma chakavu lililopo Mtaa wa Magomeni, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea Agosti 31, 2025
Amewataja waliofariki kuwa ni, Dotto Mrisho ambae alikuwa fundi wa kuchomelea mkazi wa Kichemchem na Saidi Ramadhan mkazi wa Sanzale Bagamoyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Morcase, mlipuko huo unadaiwa kusababishwa na jaribio la Dotto Mrisho (marehemu ) kukata kipande cha chuma, kitendo kilichochochea mlipuko wenye nguvu kubwa.
Mbali na kusababisha vifo na majeruhi, mlipuko huo pia umeharibu nyumba kadhaa zilizokuwa jirani na eneo la tukio, na hivyo kusababisha hasara kubwa ya mali pamoja na kuibua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Kamanda Morcase ameeleza, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
