Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mgombea urais wa Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya amekua wa 12 , leo Agosti 13, 2025, kuchukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, akiambatana na mgombea mwenza Sadous Abrahaman Khatib.

Akizungumza na Waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, Mluya amebainisha kuwa umefika wakati wa kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kwa kuyashughulikia masuala nyeti yanayogusa maisha ya kila siku.

Mluya ameeleza kwa kina mpango wake wa marekebisho ya mfumo wa kikokotoo cha mafao ya wastaafu, akisema mfumo wa sasa umekuwa chanzo cha kero na dhuluma kwa watumishi waliolitumikia taifa kwa uaminifu.

Amesema kikokotoo kitakachowekwa chini ya uongozi wake kitazingatia haki ya mfanyakazi kupata stahiki zake kwa kiwango kamili bila kupunguzwa kutokana na ukokotoaji unaoathiri kipato chao baada ya kustaafu.

“Kikokotoo kipya kitakuwa chombo cha kuondoa tabaka la umaskini, kujenga misingi imara ya ajira bora, na kuhakikisha kila mwajiriwa anastaafu kwa heshima na ustawi wa kifamilia,” amesema Mluya.

Aidha, ameahidi kuwa marekebisho hayo yatakwenda sambamba na mipango ya kuhakikisha waajiri wanawapatia wafanyakazi nyumba bora za kuishi, hatua itakayopunguza rushwa na kuongeza ari ya kazi.

Mluya amesisitiza kuwa chini ya uongozi wake, Serikali itawajibika kulinda haki za wastaafu kama sehemu ya mkakati wa ustawi wa kijamii.

Mbali na kikokotoo, Mluya amegusia changamoto zinazovikabili vyombo vya ulinzi na usalama, hasa Jeshi la Magereza, akibainisha kuwa nidhamu na heshima ya askari hao inapaswa kurejeshwa.

Amesema hali ya sasa imefikia kiwango ambacho askari magereza hawawezi kutofautishwa na wafungwa kutokana na mazingira duni ya kazi na changamoto za kimaadili.

“Tutaboresha mafunzo, maslahi na mazingira ya kazi ya askari magereza ili kuwajengea nidhamu, weledi na heshima ya kitaaluma,” ameahidi.

Vipaumbele vingine vilivyotajwa na mgombea huyo ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya kwa kuhakikisha huduma bora kwa mama wajawazito, kutoa bima ya afya ya bure kwa watoto wachanga kwa kipindi cha miezi mitatu, kuondoa ada ya kuhifadhi maiti kwa hoja kuwa walipakodi tayari, na kukuza kilimo endelevu kwa kuondoa jembe la mkono ili kuongeza pato la taifa.