Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Mhe. Hassani Iddi Mwamweta wamewekeana saini mkataba na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jamhuri ya Czech, Bw. Roman Glorig wa kuhuisha rasmi nafasi yake ya uwakilishi wa heshima.

Balozi Mwamweta alisaini mkataba huo Septemba 02, 2025 kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb).

Kusainiwa kwa mkataba huo na Bw. Glorig ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza ndege cha Airpalane africa limited kilichopo mkoani morogoro, ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha na kupanua wigo wa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Czech.

Hatua hii inalenga si tu kudumisha urafiki uliopo, bali pia kuchochea ushirikiano mpya katika sekta muhimu zikiwemo afya, elimu, biashara, uwekezaji, na utalii.

Kupitia ushirikiano huu, Serikali ina matarajio makubwa ya kuona ongezeko la ubadilishanaji wa ujuzi kati ya wananchi wa nchi hizi mbili, kuimarika kwa mikakati ya kutangaza bidhaa na vivutio vya utalii vya Tanzania, kuvutia wawekezaji kutoka Czech, pamoja na kuunga mkono mipango mbalimbali inayolenga kuinua ustawi wa jamii na kuchangia maendeleo endelevu.

Hatua hii pia ni ushahidi wa kuendelea kwa jitihada za Tanzania katika kuimarisha nafasi yake kimataifa, huku ikitafuta fursa mpya za kushirikiana na washirika wa maendeleo ili kunufaisha Taifa na wananchi wake.