Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Wakati changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa ikiendelea kuwakabili baadhi ya Wananchi wa mikoa ya pembezoni, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imechukua hatua ya kuwafuata wananchi huko waliko kupitia huduma za kliniki tembezi, hatua inayowaletea urahisi wa huduma za afya.

Kupitia ushiriki wao kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, MOI imefanikiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 70 waliojitokeza kupatiwa huduma za uchunguzi na ushauri wa kitaalamu, hasa kwa magonjwa ya mifupa, nyonga, magoti na mgongo.

Akizungumza na Jamhuri Media June 19,2025 kwenye maonesho hayo Dkt. Tumaini Minja, daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka MOI amesema, “Tumekutana na wananchi wengi waliokuwa wakihitaji huduma maalum ambazo kwa kawaida hupatikana Dar es Salaam pekee,.

Kupitia kliniki hii tembezi, tumewafikia wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani kwa urahisi zaidi, na bado tutaendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi lengo ni kuona wa Tanzania wananufaika na huduma za matibabu kwa urahisi na ufanisi, “ameeleza

Dkt. Minja ameongeza kuwa lengo la MOI ni kuhakikisha kuwa huduma bora za afya ya ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu na mifupa zinawafikia Watanzania wote kwa usawa.

“Tunaendelea kutoa huduma hata baada ya maonesho kumalizika, na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia na Serikali kwa kutuwezesha kufanya haya kupitia kliniki tembezi inayojumuisha madaktari bingwa mbalimbali,” ameeleza

Mbali na tiba, MOI imekuwa ikitoa elimu ya afya kwa wananchi ili kusaidia jamii kutambua mapema dalili za maradhi sugu yanayohusiana na mifupa na mgongo, na hivyo kusaidia kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa kuchelewa kutafuta tiba.

Kwa mujibu wa Mtaalamu huyo wa MOI, huduma hizo za karibu na wananchi zitakuwa endelevu, huku wito ukitolewa kwa wananchi kuchangamkia fursa kila timu ya madaktari bingwa inapokuwa katika mikoa yao.