Na Dotto Kwilasa, Jamhuri Media, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya “Gurudumu la Mama”,ambayo ni mpango maalum wa kuwawezesha waendesha Pikipiki maarufu kana Bodaboda na bajaji kupata matairi mapya kwa mpango nafuu wa kulipa kidogo kidogo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Mei 28,2025 jijini Dodoma, Senyamule amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kukomesha matumizi ya matairi chakavu yanayosababisha ajali za barabarani.

Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kutatua changamoto za vijana, huku akibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anawathamini vijana na anaendelea kutengeneza fursa nyingi kwa ajili yao.

“Ni imani yangu kwamba kupitia mpango huu, vijana mtapata suluhisho la changamoto zenu za usafirishaji na mtaongeza kipato kwa usalama na ufanisi,.

Tumeona ajali nyingi zinazosababishwa na matairi chakavu , hivyo huu ni wakati wa kufanya mabadiliko,” amesema Senyamule.

Aidha, RC Senyamule amewakumbusha waendesha bodaboda kuepuka matumizi ya pombe wakati wa kazi, akisisitiza kuwa matumizi hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha ajali zisizo za lazima.

“Matumizi ya pombe yamekuwa changamoto,Kama huwezi kuacha, basi tumia usiku, sio mchana mnapokuwa kazini,” ameonya.

Ametoa wito kwa vijana kujiunga na vyama vyao vya usafirishaji ili kupata fursa zaidi na kuaminika kwa wadau wa maendeleo.

Pia amewahimiza kuweka akiba na kuwa waaminifu kazini ili kuhakikisha maisha yao yanakuwa bora na ya kisasa.

Mratibu wa kampeni hiyo kutoka kampuni ya Road Master, Thuweni Makamba, amesema kuwa kampuni hiyo imeamua kuunga mkono juhudi za serikali chini ya Rais Samia kwa kauli mbiu ya “Gurudumu la Mama – Kwa safari ya uhakika: matairi mapya, usalama mpya. Mama ametusikia.”

Thuweni amesema Kampeni hiyo inalenga kuwafikia zaidi ya waendesha bodaboda 1,000 katika awamu ya kwanza na itaendelea nchi nzima kwa kushirikiana na vyama vya waendesha bodaboda.

Kampuni ya utengenezaji wa matairi ya Road Master ndiyo inasimamia upatikanaji wa matairi hayo kwa mfumo wa mkopo kwa udhamini wa vyama vya madereva.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini Mjini, Anthony Mavunde, amesema mpango huo unalenga kupunguza mzigo kwa madereva wa kipato cha chini ambao mara nyingi hushindwa kumudu gharama za matairi mapya.

“Mimi kama Mbunge wa Dodoma, nitahakikisha mnafanikiwa katika hili na katika kudhihirisha hili Juni 5 mwaka huu nitazindua SACCOS ya waendesha bodaboda zaidi ya 1,000 na tutaweka fedha kwenye mfuko huo ili kuwawezesha vijana kujiendeleza kiuchumi,” amesema Mavunde.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaji Jabir Shekimweri, amesema kuwa yeye ni mhanga wa ajali iliyosababishwa na tairi chakavu na hivyo anafahamu kwa undani madhara ya uzembe huo.

Ametoa rai kwa waendesha bodaboda kuwa na nidhamu ya usalama barabarani na kuhakikisha wanaendesha vyombo vilivyo katika hali nzuri.

Mwenyekiti wa bodaboda Mkoa wa Dodoma ametumia nafasi hiyo kuwataka wenzake kuzingatia sheria za barabarani na kutumia matairi mazuri ili kuepuka ajali, akisema: “Tunawasababishia abiria hasara ya kujiuguza kwa uzembe wetu.”